BENSON MATHEKA: Usalama wa kila mtahiniwa uhakikishwe katika msimu huu wa mitihani

BENSON MATHEKA: Usalama wa kila mtahiniwa uhakikishwe katika msimu huu wa mitihani

NA BENSON MATHEKA

MSIMU wa mitihani umeanza nchini.

Wanafunzi wa Gredi ya Sita, Darasa la nane na kidato cha nne wanafanya mitihani yao.

Huu ni wakati muhimu kwa wanafunzi hao ambao wamekuwa wakiandaliwa na walimu na wazazi wao kwa mitihani hiyo.

Muhimu kabisa wakati huu ni usalama wa wanafunzi hao, sio tu katika vituo vya kufanyia mitihani bali pia wakiwa nyumbani, wakienda na kutoka shuleni.

Hii ni kwa sababu wanafunzi huwa wanakabiliwa na hatari nyingi sana. Hatari hizi zinaweza kuwapata popote na ndiyo sababu usalama wao unafaa kusisitizwa na kuhakikishwa.

Kumekuwa na visa vya wanafunzi kuvamiwa na majangili wakiwa shuleni hasa maeneo ya Kaskazini mwa Bonde la Ufa.

Baadhi ya shule katika eneo hilo pia zimefungwa kufuatia kudorora kwa usalama na inasadikika serikali imefanya mipango ili watahiniwa waliokuwa wakisomea shule hizo wasikose kufanya mtihani.

Linaweza kuwa jambo la kusikitisha kwa mwanafunzi, walimu na wazazi kuweka bidii wakilenga kufanya vyema katika mitihani kisha wakose kuifanya kwa sababu ya ghasia zinazosababishwa na wahalifu.

Serikali itakuwa imefeli pakubwa iwapo kutaripotiwa kisa cha mwanafunzi kukosa haki yake ya kufanya mtihani wa kitaifa kwa kuhofia usalama wake. Hili ni suala la Wizara ya Usalama wa Ndani na Elimu.

Bila shaka kuna usalama wa mitihani yenyewe ambao pia unafaa kuhakikishwa. Usalama wa mitihani unahakikisha usawa kwa watahiniwa wote lakini ukikumbwa na udanganyifu huwa umepoteza uadilifu.

Vile vile, kwa kuwa mitihani ya mwaka huu inafanyika katika mazingira magumu kutokana na ukame wa muda mrefu katika maeneo mengi, watahiniwa wote wanafaa kupewa chakula siku ambazo watakuwa wakifanya mitihani yao. Kwa kufanya hivi, serikali itakuwa imesaidia wanafunzi wengi ambao huenda wangekosa umakinifu kwa sababu ya njaa.

  • Tags

You can share this post!

Cherera afeli kufika mwenyewe mbele ya JLAC

CHARLES WASONGA: Mpango wa kuwapa machifu bunduki...

T L