BENSON MATHEKA: Vijana wapuuze wanasiasa wakiwachochea kuzua ghasia wakati wa uchaguzi

BENSON MATHEKA: Vijana wapuuze wanasiasa wakiwachochea kuzua ghasia wakati wa uchaguzi

NA BENSON MATHEKA

SIKU ya leo ni muhimu kwa nchi ya Kenya na raia wake.

Wakenya zaidi ya 22 milioni wameraukia katika vituo vya kupigia kura kote nchini kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa miaka mitano ijayo kuanza mbunge wa wadi katika mabunge ya kaunti, Mwakilishi wa Kike, Mbunge, Seneta, Gavana na Rais.

Kwa ufupi, uchaguzi mkuu nchini Kenya huwa ni wa kuchagua watakaoshikilia nyadhifa sita kuanzia mashinani hadi kitaifa.

Hivyo basi, ni makosa makubwa kwa mtu aliye na afya nzuri kukataa kwenda kupiga kura ikizingatiwa kuwa serikali imetenga siku ya leo kuwa sikukuu ili kupatia kila mmoja fursa ya kutekeleza haki yake ya demokrasia.

Muhimu kabisa kwa watakaopiga kura, ni kudumisha nidhamu ya hali ya juu. Nidhamu hii sio tu katika vituo vya kupiga kura mbali ni hata baada ya matokeo kutangazwa. Inafaa kubainika kuwa baadhi ya wagombeaji huwa wanatumia mbinu chafu wanapohisi wanashindwa au wakishindwa kwenye uchaguzi.

Sio mara ya kwanza wanasiasa kuchochea wafuasi wao ili wazushe ghasia kwa lengo la kutimiza malengo yao ya kibinafsi. Ni mbinu hizi za kulipa vijana wazue fujo zinazosababisha ghasia na mauaji kila baada ya uchaguzi mkuu.

Hata hivyo, vijana wanaweza kufanya uchaguzi wa mwaka huu kuwa tofauti na kuweka Kenya katika orodha ya nchi ambazo zimekomaa kidemokrasia.

Vijana wanafaa kuwakumbusha wanasiasa wanaowashawishi kuzua ghasia ahadi yao ya kudumisha amani ambayo walikuwa wakitoa wakati wa kampeni zao na kwenda nyumbani baada ya kupiga kura kusubiri matokeo.

Wito wa baadhi ya wanasiasa kuwataka vijana kulinda kura ni wa kuwachochea na wanafaa kuukataa kwa kuwa wanaowahimiza, kuwalipa na kuwarai kuzua fujo hawawezi kuruhusu watoto wao kufanya hivyo. Tupige kura na kudumisha amani ili tuwe mfano mwema Afrika na duniani kote.

  • Tags

You can share this post!

Usalama kuimarishwa Kerio Valley

TAHARIRI: Kususia kura si jibu la kupata uongozi bora

T L