BENSON MATHEKA: Viongozi wanawake waungwe mkono ili wafaulu kutekeleza majukumu yao

BENSON MATHEKA: Viongozi wanawake waungwe mkono ili wafaulu kutekeleza majukumu yao

NA BENSON MATHEKA

IDADI ya wanawake walioshinda viti vya uongozi kwenye uchaguzi mkuu wa wiki jana imeongezeka na kutia moyo kwamba Wakenya wanakubali mchango wa wanawake kwa maendeleo ya nchi.

Kutakuwa na magavana saba wanawake kati ya 47 wa kaunti nchini kwa miaka mitano ijayo na Wakenya wameonyesha kwamba wanaamini wanawake kwa kuwachagua kuwa wabunge na madiwani.

Hata hivyo, itabidi wanawake hao waungwe mkono na Wakenya, wakiwemo viongozi wanaume katika maeneo yao na kitaifa ili waweze kufaulu katika majukumu yao.

Kumekuwa na mtindo wa wanaume kuhujumu viongozi wanawake ili waonekane duni na kushindwa katika majukumu yao ya kuhudumia raia. Kasumba hii imepitwa na wakati na raia waliowachagua viongozi hao wanawake wanapaswa kuwalinda dhidi ya njama kama hizo.

Hapa, ninataka kufafanua kuwa ulinzi huu ni kwa wale watakaotimiza ahadi zao kwa wapigakura lakini sio kwa wale watakaopotoka na kutumia vibaya mamlaka ya ofisi zao.

Kwa kuwabwaga wanaume waliokuwa wakishindana nao, viongozi hao walidhihirisha kuwa wana nguvu, uwezo, akili na ujuzi wa uongozi na wanafaa kupatiwa nafasi ya kutekeleza ajenda zao za maendeleo kwa manufaa ya raia.

Hii haimaanishi kuwa wasikosolewe wanapovuka mipaka au wanapoenda kinyume cha katiba na maadili. Wanaowakosoa wanapaswa kufanya hivyo kwa kutumia mbinu za heshima.

Makosa makubwa ambayo viongozi wamekuwa wakifanya ni kulewa na mamlaka na kusahau kwamba nia ya raia kuwachagua ni kuwahudumia.

Tunataka kuona uongozi wa wanawake ulio tofauti na wa wanaume na hii itawezekana wasipokubali kulewa na mamlaka na wasipokubali kutumiwa na vibaraka wao na wasipoingiwa na tamaa ya kupora mali ya umma.

Ni kufaulu kwa viongozi wanawake hasa waliochaguliwa magavana ambako kutafungua milango ya wenzao wengi kushinda viti kwenye chaguzi zijazo.

  • Tags

You can share this post!

Raila apinga matokeo ya IEBC

Hesabu yakanganya makamishna walioasi matokeo ya urais

T L