BENSON MATHEKA: Wagombeaji wa kiume wazuiwe kuwadhalilisha wa kike

BENSON MATHEKA: Wagombeaji wa kiume wazuiwe kuwadhalilisha wa kike

Na BENSON MATHEKA

Zimebaki siku 13 wapigakura Kaunti ya Machakos wamchague seneta wao kujaza kiti kilichobaki wazi kufuatia kifo cha Seneta Bonface Kabaka mwaka jana.

Wagombeaji wa vyama tofauti wamekuwa wakifanya kampeni kali ilivyo kawaida wakati wa maandalizi ya uchaguzi.

Orodha ya wagombeaji inaonyesha kuwa wanaume ni wengi kuliko wanawake.

Hili sio Jambo geni katika siasa za uchaguzi nchini ambapo ni wanawake wachache wanaojitokeza kugombea viti mbalimbali.

Japo kuna wagombeaji tisa walioidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kugombea kiti hicho, ushindani mkali unaonekana kuwa kati ya John Katuku wa chama cha Maendeleo Chap Chap, Urbanus Ngengele wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) na Agnes Kavindu wa chama cha Wiper.

Hata hivyo, kinachoshangaza ni kuwa badala ya wagombeaji hao hasa wanaume kuuza sera kwenye kampeni zao kwa wapigakura wamezibadilisha kuwa dhuluma za jinsia kwa kuwadhalilisha wagombeaji wanawake.

Si mara moja wamesikika wakiwataka wapigakura kuwakataa wagombeaji wanawake wakisema wanafaa kufanya kazi za nyumbani.

Baadhi yao wameingilia maisha ya kibinafsi, ndoa na familia ya wagombeaji wanawake.

Hizi ni fikira na mbinu duni za watu wasio na maono yoyote kwa wapigakura wengi ambao ni wanawake.

Kauli za wanasiasa hao zinaonyesha ukosefu wa ukomavu wa masuala yanayoathiri jamii na hasa wakazi wa Machakos ambao wanataka seneta atakayehakikisha kuwa pesa zinazotengewa kaunti yao zitatumika vyema, kwamba serikali ya kaunti itatekeleza majukumu yake kwa uwazi na kushirikisha umma na kwamba rasilmali za kaunti ikiwemo ardhi yao imelindwa vyema.

Madai ya baadhi ya wagombeaji kwamba wenzao wa jinsia tofauti na yao hawafai kuchaguliwa ni sawa na kuendeleza dhuluma za kijinsia ambazo viongozi kote ulimwenguni wamekuwa wakipigana kuangamiza.

Kampeni za kuumbuana na kupakana tope zinaonyesha kuwa wagombeaji hawana sera zozote za kuwafaidi wapigakura.

Wanawake wana haki sawa na wanaume katika masuala ya uongozi na hawafai kudhalilishwa wanapojitokeza kugombea nyadhifa.

Hawafai kutusiwa, kutishwa na kudhalilishwa kamwe na wanaofanya hivi wanaonyesha kwamba hawafai kuwa viongozi.

Mashindano ya kisiasa yanafaa kuwa kwa manifesto ya kila mgombeaji na sio uzito wa matusi na vitisho anavyorushia wapinzani wake.

Kuchagua mwanasiasa anayedhalilisha jinsia moja ni kuendeleza dhuluma za jinsia

You can share this post!

MAUYA OMAUYA: Serikali idhibiti wanabodaboda, vinginevyo...

WANDERI KAMAU: Hukumu ya Sarkozy isaidie Waafrika kufunguka...