BENSON MATHEKA: Wakenya wasisubiri muujiza kutoka kwa serikali ya Ruto, lazima watoe jasho

BENSON MATHEKA: Wakenya wasisubiri muujiza kutoka kwa serikali ya Ruto, lazima watoe jasho

NA BENSON MATHEKA

MAONI mseto yametolewa kuhusu maamuzi ya Rais William Ruto wiki moja baada ya kuapishwa na kuingia mamlakani.

Kuna wanaounga maamuzi yake kama vile kuapisha majaji sita ambao mtangulizi wake Uhuru Kenyatta alikuwa amewakataa.

Vilevile, Wakenya wamekuwa na maoni tofauti kuhusu hatua ya Rais Ruto ya kuondoa ruzuku ya mafuta na unga wa mahindi na kukataa kata kata kushirikiana na upinzani.

Kuna wanaomuunga mkono wakisema ameenda kinyume na ahadi zake wakati wa kampeni, kwamba angepunguza gharama ya maisha inayowalemea Wakenya wengi.

Kwa upande mwingine kunao wanamtetea wakisema ni mapema kupima utendakazi wake kwa kuwa amerithi nchi wakati ambao mfumko wa maisha uko juu.

Ni haki ya kikatiba ya kila Mkenya kutoa maoni. Katika demokrasia, maoni kama haya husaidia serikali kurekebisha sera zake yakitolewa kwa mfumo uliowekwa katika Katiba.

Yote tisa kumi ni kuwa Rais William Ruto wa Jamhuri ya Kenya ni tofauti na mgombea urais William Ruto aliyekuwa akizunguka kote amevalia sare za manjano za chama chake cha United Democratic Alliance (UDA).

Manifesto ambayo baadhi ya wanaokosoa maamuzi wake wanataja ilikuwa stakabadhi ya kampeni ambayo kwa kawaida huwa ahadi ambazo wapigakura hutaka kusikia.

Ahadi hizo huwa zimepambwa kwa lugha ya kuwavutia wapigakura fufufu. Baada ya kutangazwa mshindi na kuvaa suti za kisasa na jozi la viatu vinavyong’ara, Rais Ruto, ni lazima aandae stakabadhi za kazi kwa kutegemea ukweli na uhalisi wa mambo.

Kwa sasa miujiza aliyokuwa akiahidi wakati wa kampeni haitathubutu, pengine baadaye. Ikija, mahasla waliokuwa wakisubiri watasema hewala!

La busara kwao ni kuanza kuzoea hali halisi, wakishukuru kwa mazuri yakiwafikia hata kama ni makombo watakayolazimika kutoa jasho kupata.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi Ruto alivyosafirishwa kama hasla London Malkia...

CHARLES WASONGA: Bei ya Sh3,500 ya mbolea si afueni tosha...

T L