Bensouda afurahia kuruhusiwa kukagua vifaa vilivyomilikiwa na wakili Gicheru

Bensouda afurahia kuruhusiwa kukagua vifaa vilivyomilikiwa na wakili Gicheru

Na VALENTINE OBARA

AFISI ya Kiongozi wa Mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) inayoongozwa na Bi Fatou Bensouda, imepata ushindi wake mkubwa wa kwanza dhidi ya wakili Paul Gicheru aliyejisalimisha mwaka uliopita.

Bw Gicheru angali amezuiliwa ICC kwa madai ya kushawishi mashahidi wajiondoe katika kesi iliyomwandama Naibu Rais, Dkt William Ruto na mwanahabari Joshua Sang kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Mahakama imeamua kwamba afisi ya Bi Bensouda ikabidhiwe vifaa vitano ambavyo havijatajwa, vinavyomilikiwa na wakili huyo ambavyo alikuwa amewasili navyo jijini The Hague (Uholanzi) alipojisalimisha.

Imebainika polisi wa Uholanzi walimpekua Bw Gicheru alipofika nchini humo na wakampata na vitu mbalimbali, vikiwemo vitano ambavyo waliamua kuviweka kando.

Walipomwasilisha kwa ICC, maafisa katika kitengo cha usajili wa mahakama waliamua kuhifadhi vitu hivyo vitano, na kuwasilisha ombi kwa Jaji Reine Alapini-Gansou anayesikiliza kesi hiyo atoe mwelekeo kuhusu wanachofaa kuvifanyia.

Bi Bensouda aliwaomba majaji, aruhusiwe kuvikagua ili atumie chochote atakachopata kuimarisha ushahidi wake, lakini wakili Michael Karnavas, anayemwakilisha Bw Gicheru, akapinga ombi hilo akisema litaingilia mambo ya siri ya mteja wake.

Mnamo Jumatatu jioni, Jaji Gansou alitoa uamuzi kwamba aliridhishwa na ombi la Bi Bensouda na hivyo akatupilia mbali ombi la Bw Gicheru kutaka arudishiwe mali yake bila kuchunguzwa.

Kulingana na jaji huyo, makosa ambayo Bw Gicheru anashtakiwa nayo ni mazito na yanahusu mtandao mkubwa wa kihalifu uliotumiwa tangu Aprili 2013 kushawishi mashahidi kujiondoa katika kesi za uhalifu dhidi ya haki za binadamu.

“Kiongozi wa mashtaka ana jukumu kuchunguza vifaa hivi kwa msingi wa kanuni za kisheria za mahakama, na ikiwezekana, mlalamishi anaweza kutaja masuala yoyote yatakayoibuka baadaye kuhusu suala hili wakati kesi itakapokuwa ikiendelea,” akasema Jaji katika uamuzi wake.

Jaji huyo alieleza kuwa, uamuzi huo ulizingatia agizo lililokuwa limetolewa awali la kukamatwa kwa Bw Gicheru pamoja na mshukiwa mwingine, Philip Kipkoech Bett kwa madai ya kuhujumu utendaji wa haki kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi.

Alisema, katika agizo la kukamatwa kwao lilihitaji wapekuliwe pamoja na sehemu ambapo wangekamatwa ikiwemo nyumba au afisi zao, na chochote ambacho kingeaminika kinaweza kutegemewa kama ushahidi kiwasilishwe mahakamani.

Bw Gicheru alijisalimisha kwa ICC mnamo Novemba 2, akafikishwa mbele ya mahakama Novemba 6 ambapo alikana kuhusika katika madai yaliyotolewa dhidi yake.

Ijapokuwa aliomba kuachiliwa huru, kesi yake ikiendelea na upande wa mashtaka haukupinga ombi hilo, Serikali ya Kenya ilikataa kujihusisha na kesi yake na hivyo basi kufanya aendelee kukaa kizuizini The Hague.

Hali hii ni kutokana na kuwa, serikali inahitajika kuahidi kuwa itasaidia mahakama hiyo kuendeleza kesi hiyo, ikiwemo kwa kurahisisha safari zake kati ya Kenya na Uholanzi.

Kupitia kwa Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki, Serikali ilisema Bw Gicheru hakufuata sheria za nchi alipojisalimisha na hivyo basi Kenya itakuwa inakiuka sheria ikijihusisha na kesi hiyo.

You can share this post!

Hotuba ya Uhuru yazidisha nyufa katika ngome yake

Msimu wa utapeli waanza