Michezo

Benzema abeba Real Madrid hadi hatua ya 16-bora UEFA

December 10th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MABAO ya kichwa kupitia kwa Karim Benzema yaliwezesha Real Madrid kupepeta Borussia Monchengladbach ya Ujerumani 2-0 mnamo Disemba 9, 2020 na kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

M’gladbach pia walifuzu kwa hatua hiyo ya mwondoano baada ya Inter Milan ya kocha Antonio Conte kuambulia sare tasa katika mechi nyingine ya Kundi B iliyowakutanisha na Shakhtar Donetsk ya Ukraine uwanjani San Siro, Italia.

Real ambao ni mabingwa mara 13 wa taji la UEFA, walianza mchuano wao dhidi ya M’gladbach wakishikilia nafasi ya tatu kundini na kwenye hatari ya kubanduliwa kwenye hatua ya makundi kwa mara ya kwanza katika historia ya kushiriki kwao kipute hicho.

Mabao yaliyopachikwa wavuni na Benzema yalikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Lucas Vazquez na chipukizi Rodrygo.

Real walianika kiu yao ya kushinda mechi hiyo mapema huku wakitamalaki mechi na kuwazidia maarifa wageni wao katika kila idara.

Kikosi hicho cha kocha Zinedine Zidane kingalifunga idadi kubwa zaidi ya mabao ila refa akakataa kuhesabu goli la Luka Modric kwa madai kwamba alikuwa ameotea huku Benzema na Vazquez wakishuhudia makombora yao ya dakika za mwisho yakigonga mwamba wa lango la M’gladbach.

Real kwa sasa wamefuzu kwa hatua ya 16-bora ya UEFA katika kipindi cha miaka 25 iliyopita tangu 1996-97 ambapo walishindwa kufuzu kushiriki hata hatua ya mchujo ya soka hiyo.

Miamba hao wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), sasa wamejizolea mataji manne ya UEFA katika kipindi cha misimu saba iliyopita.

Masogora wa Real walishuka dimbani wakitawaliwa na ari ya kushinda M’gladbach baada ya kupokezwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Shakhtar mnamo Disemba 1, 2020 uwanjani Alfredo di Stefano.