Benzema sasa kuchezea Ufaransa kwa mara ya kwanza tangu 2015

Benzema sasa kuchezea Ufaransa kwa mara ya kwanza tangu 2015

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI wa Real Madrid, Karim Benzema amejumuishwa katika kikosi cha wanasoka 26 kitakachotegemewa na Ufaransa kwenye fainali zijazo za Euro.

Fainali hizo zilizoahirishwa mwaka wa 2020 sasa zitafanyika kati ya Juni na Julai 2021.

Benzema anajumuishwa katika timu ya taifa ya Ufaransa kwa mara ya kwanza baada ya kuwa nje kwa takriban miaka sita. Fowadi huyo hajawahi kuchezea Ufaransa tangu 2015 baada ya kudaiwa kuhusika kwenye tukio la utapeli lililomhusisha aliyekuwa mchezaji mwenzake kambini mwa Ufaransa.

Benzema, 33, alikosa kuwajibikia Ufaransa kwenye fainali za Euro 2016 na Kombe la Dunia 2018 kutokana na madai hayo dhidi yake.

Mnamo Januari 2021, waendeshaji mashtaka nchini Ufaransa walitangaza kwamba Benzema atashtakiwa.

Benzema anatuhumiwa kulipa baadhi ya watu kumtishia kiungo Mathieu Valbuena, 36, mnamo 2015 ili awape kiasi kikubwa cha fedha au la wafichue kanda za ngono zilizomhusisha mwanasoka huyo.

Baada ya kuthibitisha kwamba Benzema atakuwa sehemu ya kikosi chake kwenye fainali zijazo za Euro, kocha Didier Deschamps alisema: “Kitu muhimu zaidi ni leo na kesho.”

“Kulikuwapo na hatua muhimu. Tulionana uso kwa macho. Nilijadiliana na Benzema kwa kina. Nilitathmini upya masaibu yanayomkumba na nikafanya maamuzi. Sitafichua lolote kuhusu mazungumzo yetu ila najua yalikuwa muhimu kwangu na kwa Benzema pia,” akaongeza mkufunzi huyo.

Picha mseto Mei 18, 2021 kuonyesha timu ya Ufaransa ya fainali za Euro 2020 (Kushoto hadi Kulia, Juu hadi Chini) magolikipa Hugo Lloris, Mike Maignan, Steve Mandanda, mabeki Lucas Digne, Leo Dubois, Lucas Hernandez, Presnel Kimpembe, Jules Koundee, Clement Lenglet, Benjamin Pavard, Raphael Varane, Kurt Zouma, viungo N’Golo Kante, Thomas Lemar, Paul Pogba, Adrien Rabiot, Moussa Sissoko, Corentin Tolisso na wavamizi Wissam Ben Yedder, Karim Benzema, Kingsley Coman, Ousmane Dembele, Olivier Giroud, Antoine Griezmann, Kylian Mbappe na Marcus Thuram. Picha/ AFP

Hugo Lloris na Moussa Sissoko wa Tottenham Hotspur, beki wa kushoto Lucas Digne wa Everton, Kurt Zouma, Olivier Giroud na N’Golo Kante wa Chelsea pamoja na Paul Pogba wa Manchester United ni miongoni mwa masogora wanaosakata soka ya kulipwa nchini Uingereza ambao watakuwa kambini mwa kikosi cha Ufaransa.

Ufaransa wametiwa katika Kundi F kwenye fainali za Euro kwa pamoja na Hungary, Ujerumani na mabingwa watetezi Ureno. Hilo ndilo kundi gumu zaidi kwenye mapambano hayo.

Kufikia sasa, Benzema amepachika wavuni jumla ya mabao 27 kutokana na mechi 81 ambazo amechezea Ufaransa. Alifunga magoli mawili mara ya mwisho alipochezea Ufaransa katika ushindi wa 4-0 dhidi ya Armenia kirafiki.

Amekuwa miongoni mwa wanasoka tegemeo zaidi kambini mwa Real msimu huu na amefunga mabao 29 yakiwemo 11 kutokana na mechi 10 zilizopita. Amechangia pia jumla ya magoli manane kwenye mashindano yote.

Chini ya kocha Zinedine Zidane, Real wanapanga kuwaruka viongozi wa jedwali Atletico Madrid na kutia kapuni taji lao la 35 kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga). Imesalia mechi moja pekee kwa kipute hicho msimu huu kukamilika rasmi.

Huu ukiwa mwaka wake wa 12 wa kuchezea Real ugani Santiago Bernabeu, Benzema alitawazwa Mchezaji Bora raia wa Ufaransa anayechezea ugenini. Aliibuka mshindi wa tuzo hiyo iliyodhaminiwa na Muungano wa Wanasoka Wataalamu wa Kitaifa Nchini Ufaransa (FNUPFP).

Ujio wa Benzema kambini mwa Ufaransa unatarajiwa kupiga jeki safu ya mbele ya kikosi hicho ambacho tayari kinajivunia huduma za wanasoka Kylian Mbappe wa Paris Saint-Germain (PSG) na Antoine Griezmann wa Barcelona.

Timu ya taifa ya Ufaransa almaarufu ‘The Les Bleus’ ilitinga fainali ya makala yaliyopita ya Euro yaliyoandaliwa nchini Ufaransa mnamo 2016. Hata hivyo, walizidiwa ujanja na Ureno waliowapiga 1-0 kupitia goli la Eder Macedo Lopes wa klabu ya Lokomotiv Moscow nchini Urusi.

Ufaransa waliotawazwa mabingwa wa dunia mnamo 2018 nchini Urusi, wameratibiwa kuanza kampeni zao za Euro dhidi ya Ujerumani mnamo Juni 15. Ujerumani waliibuka wafalme wa Kombe la Dunia mnamo 2014 nchini Brazil.

KIKOSI CHA UFARANSA:

MAKIPA: Hugo Lloris (Tottenham), Mike Maignan (Losc), Steve Mandanda (Marseille).

MABEKI: Lucas Digne (Everton), Leo Dubois (Lyon), Lucas Hernandez (Bayern Munich), Presnel Kimpembe (PSG), Jules Kounde (Sevilla), Clement Lenglet (Barcelona), Benjamin Pavard (Bayern Munich), Raphael Varane (Real Madrid), Kurt Zouma (Chelsea).

VIUNGO: N’Golo Kante (Chelsea), Thomas Lemar (Atletico Madrid), Paul Pogba (Manchester United), Adrien Rabiot (Juventus), Moussa Sissoko (Tottenham), Corentin Tolisso (Bayern Munich).

WAVAMIZI: Wissam Ben Yedder (Monaco), Karim Benzema (Real Madrid), Kingsley Coman (Bayern Munich), Ousmane Dembele (Barcelona), Olivier Giroud (Chelsea), Antoine Griezmann (Barcelona), Kylian Mbappe (PSG), Marcus Thuram (Borussia Monchengladbach).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Rais Biden sasa ataka Israeli isitishe mashambulio Gaza

Wabunge kukutana kujadili na kupigia kura ripoti kuhusu...