Michezo

Berlin FC mabingwa wa Chapa Dimba Kaskazini Mashariki

April 24th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Berlin FC ilionyesha weledi wake na kutwaa ubingwa wa Chapa Dimba na Safaricom Season Two katika Mkoa wa Kaskazini Mashariki ilipoikomoa Al-Ansar kwa magoli 4-3 kupitia mikwanju ya penalti kwenye fainali iliyoandaliwa Garissa University mjini humo.

Berlin FC ilitawazwa mabingwa wa mkoa huo ilipotandika Al-Ansar FC kwa mabao 4-3 kupitia penalti baada ya kutoka sare tasa katika muda wa kawaida.

Timu hizo zilionyesha mechi ya kusisimua kila moja ikilenga kuibuka mabingwa wa huo na kunasa tiketi ya kushiriki fainali za kitaifa mwaka huu zitakazoandaliwa Kinoru Stadium, Kaunti ya Meru.

Naye Yahya Mohamed Abdi wa Berlin FC alitawazwa mlinda lango bora huku Abdallah Marro (Berlin FC), Ahmed Adan (Al-Ansar FC) na Ahmed Abdihakim (Jamia FC) wote wakitawazwa wafungaji bora baada kila mmoja kutikisa wavu mara moja. Tuzo ya mchezaji bora ilimwendea mchana nyavu, Abdallah Marro wa Berlin FC.

Kando na tiketi ya kufuzu kushiriki fainali za kitaifa, Berlin FC pia ilituzwa kitita cha Sh200,000 huku Al-Ansar ikipongezwa kwa Sh100,000.

”Tunamshukuru Mungu tumeibuka mabingwa wa Mkoa huu sasa tunalenga kubeba ubingwa wa kitaifa,” Abdallah Marro mchezaji bora kwenye michezo hiyo alisema.

Kikosi hicho sasa kimejiunga na mabingwa kutoka Mikoa mingine ikiwamo: Super Solico Boys-wavulana na St Marys Ndovea-wasichana (Mashariki) Al Ahly na Kitale Queens wavulana na wasichana(Rift Valley), Lugari Blue Saints (wavulana) na Bishop Njenga Girls (Magharibi), Manyatta Boys na Ndhiwa Queens(Nyanza), Shimanzi Youth-wavulana na Changamwe Ladies(Mombasa) bila kusahau Euronuts Boys na Barcelona Ladies (Mkoa wa Kati). Mabingwa wa kitaifa timu ya wavulana pia wasichana kila moja itatuzwa kitita cha Sh 1 milioni.