Michezo

Berlin FC macho kwa taji la Chapa Dimba

June 2nd, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

BERLIN FC inalenga kujituma mithili ya mchwa kuhakikisha imefuzu kushiriki mechi ya fainali kufukuzia taji la Chapa Dimba na Safaricom Season Two mwaka huu kwenye fainali za kitaifa zitakazopigiwa uwanjani Kinoru Stadium, mjini Meru.

Kocha wake, Ahmed Mohamed Hirmoge anasema kuwa ingawa ndiyo mwanzo kufuzu kwa fainali za kitaifa anaamini vijana wake wanatosha kuvuruga matumaini ya wapinzani wao.

”Tumepania kutimiza mambo mawili kwenye kipute hicho, kwanza kufuzu kwa fainali na kuibuka mabingwa la sivyo kumaliza nafasi ya pili,” alisema.

Wavulana hao walionyesha weledi wao na kutwaa tikiti ya kuwakilisha Mkoa wa Kaskazini Mashariki kwenye ngarambe hiyo walipolima Al-Ansar kwa magoli 4-3 kupitia mikwanju ya penalti katika fainali iliyopigiwa Garissa Teachers Training College (GTTC).

”Wachezaji wangu wanaendelea na mazoezi kujiandalia mtanange huo utaofanyika mwishoni mwa mwezi huu,” alisema na kuongeza kwamba angependa sana mchezo wa kwanza kukutanishwa na Manyatta Boys ya Nyanza inayopigiwa upatu kutesa kwenye mechi hizo.

Berlin FC iliibuka mabingwa wa Mkoa huo bila kupoteza mchezo wowote hali inayodhihirisha kwamba wachezaji hao wamejipanga kinoma. Matokeo ya mechi za kuanzia mashinani yalikuwa hivi: Berlin FC 6-0 Balambala FC, Berlin FC 5-0 Fafi FC, Berlin FC 4-1 White Eagles, Berlin FC 1-0 Blackstars, pia ilinasa ufanisi wa mechi tatu kwa mabao 2-0 kila moja mbele ya Dutch FC, Red Eagles na MO-Town.

Kwenye fainali za mkoa huo, Yahya Mohamed Abdi wa Berlin FC alitawazwa mlinda lango bora huku Abdallah Maro (Berlin FC), Ahmed Adan (Al-Ansar FC) na Ahmed Abdihakim (Jamia FC) wote wakitawazwa wafungaji bora baada kila mmoja kutikisa wavu mara moja.

Tuzo ya mchezaji bora ilimwendea mchana nyavu, Abdallah Maro wa Berlin FC. Kadhalika wachezaji watatu waliteuliwa katika kikosi cha timu ya taifa kilichokuwa nchini Uhispania kwa mafunzo ya mchezo huo. Chipukizi hao ni Issa ‘Mutu’ Minhaj, Khalida Yussuf Behei na Abdalla Maro.

Berlin FC inayolenga kuibuka kati ya vikosi mahiri katika mkoa huo inajumuisha wachezaji kama: Yahya Mohamed, Warsame Hassan, Athman Maro, Mohamed Sheikh, Feisal Guhad, Idris Bawata, Abdinassir Ali, Khalid Yussuf, Issa Minhaj, Kahin Noor na Abdalla Maro.

Pia wapo Abubakar Adan, Jaafar Mohamed, Dasho Abdiaziz, Timothy Simiyu, Liban Abdirahman, Abdiwali Mohamed, Salat Ibrahim na meneja wa timu Ali Olow.

Mabingwa wa taji hilo kutoka Mikoa mingine waliofuzu kwa fainali za kitaifa wanajumuisha:Super Solico Boys-wavulana na St Marys Ndovea-wasichana (Mashariki) Al Ahly na Kitale Queens wavulana na wasichana(Rift Valley), Lugari Blue Saints (wavulana) na Bishop Njenga Girls(Magharibi), Manyatta Boys na Ndhiwa Queens(Nyanza), Shimanzi Youth-wavulana na Changamwe Ladies(Mombasa), Euronuts Boys na Barcelona Ladies (Mkoa wa Kati) na Acakoro Ladies (Mkoa wa Nairobi).