Michezo

Bernado Silva amtema Alicia

June 25th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO Bernardo Silva wa Manchester City, amethibitisha kwamba amepata hifadhi mpya ya penzi lake moyoni mwa mwanamitindo mzawa wa Ureno, Ines Degener Tomaz.

Mwishoni mwa mwezi jana, Silva, 25, alipakia mtandaoni picha iliyopigwa akiwa na Ines nje ya kasri lake jijini Lisbon, Ureno. Tukio hilo lilikuwa ithibati kuwa alikuwa ametemana kabisa na mrembo Alicia Verrando aliyevurugana naye miaka miwili iliyopita.

Kwa upande wake, Ines ambaye dada yake, Mariana aliwakilisha Ureno katika shindano la Miss Global 2017, alipakia mtandaoni video iliyomwonyesha akimshika Silva kiuno na kidevu kwenye ufuo wa Ibiza, Uhispania.

Video hiyo ilikuwa jibu kwa nyingine iliyopakiwa na Silva kwenye Instagram akimbusu Ines huku akiyapapasa maziwa yake kifuani katika mkahawa mmoja wa kifahari.

Mmojawapo wa mashabiki wa Silva aliandika, “Wewe ni jogoo kamili. Unawika uwanjani na chumbani pia. Hongera!” Mwingine alisema: “Heko kaka kwa uchawi wa kuteua videge vya kutamanisha kiasi kile.”

Wengine waliomhongera Silva kwa kujinasia demu mpya ni rafiki wa karibu wa Ines, Madalena Bonvalot ambaye pia ni mwanamitindo maarufu mjini Monte Carlo, Ufaransa.

Japo Silva na Ines hawakufichua wakati kamili walipoanza kutoka kimapenzi, inakisiwa kwamba wawili hao walianza kula bata miezi mingi iliyopita ila uhusiano wao ukawa wa siri.

Kuyeyuka kwa mapenzi kati ya Silva na Alicia kulichangiwa na jicho la nje la sogora huyo alyehamia jijini Manchester, Uingereza mnamo 2017 na kumwacha Alicia jijini Monaco, Ufaransa.

Alicia aliyewahi kuwa afisa wa mauzo kambini mwa AS Monaco, alikutana na Silva kwa mara ya kwanza mnamo 2017. Wakati huo, Silva alikuwa mchezaji wa kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Ufaransa. Kukomaa kwa penzi lao kulidhihirika mnamo 2018 baada ya Alicia kutua nchini Urusi kushabikia timu ya taifa ya Ureno kwenye mechi ya fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Uruguay.

Hata hivyo, uhusiano wao ulianza kuwa baridi na walionekana pamoja mara ya mwisho mnamo Juni 2018 katika mkahawa wa Sesimbra viungani mwa jiji la Lisbon, Ureno. Alicia anadai kuwa huo ndio wakati wa kwanza kwa Silva kulitikisa buyu lake la asali.

Baada ya hapo, Silva alianza kuwa mwepesi wa kupakia mitandaoni picha za harusi ya dada yake, Maria, badala ya zile alizopigwa na Alicia katika sehemu mbalimbali za burudani.

Alicia ambaye ni mwanafunzi wa zamani wa masuala ya biashara za kimataifa katika Chuo Kikuu cha California, Amerika pia anajivunia umilisi mkubwa wa lugha za Kiingereza, Kireno na Kifaransa. Nyingi za filamu zake za uanamitindo zimefyatuliwa katika mataifa ya Cuba na Morocco na mjini Rio de Janeiro, Brazil.