Besigye achemkia Museveni kupanda kwa visa vya corona

Besigye achemkia Museveni kupanda kwa visa vya corona

Na DAILY MONITOR

KAMPALA, Uganda

KIONGOZI mkongwe wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, amekashifu vikali utawala wa Rais Yoweri Museveni kwa kukosa kumakinikia vita dhidi ya corona, huku janga hilo likiendelea kusambaa kwa kasi katika taifa hilo.

Besigye, ambaye hakuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, alidai kuwa Museveni anatumia suala hilo kuhadaa raia ili kujijenga kisiasa, badala ya kuweka mikakati kabambe ya kupigana na virusi hivyo hatari.

Uganda kwa sasa imefungwa kwa siku 42, hatua iliyochukuliwa na serikali kama njia ya kuzuia kuenea kwa maambukizi zaidi ya ccorona.

“Tangu kisa cha kwanza cha corona kiripotiwe Machi 2020, kumeibuka masuala mengi, hususan jinsi maambukizi yanaweza kudhibitiwa.

“Serikali, hata hivyo, ilipuuza ushauri wa wataalamu wa afya na sasa raia wanaumia kutokana na hali ambayo ingeepukika,” alisema Besigye kwenye kikao na wanahabari katika afisi zake zilizoko kwenye barabara ya Katonga jijini Kampala.

Aliongeza: “Kwa sasa Uganda inaishiwa na nguvu katika vita dhidi ya janga hilo ambalo masambao wake umeingia wimbbi la nne. Maambukizi yameongezeka mno katika jamii tangu mwezi uliopita.”

Besigye amekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Rais Museveni kwa miaka mingi.

Maafa ambayo yamesababishwa na virusi vya corona Uganda yalikuwa watu 1,023 kufikia jana.

Maambukizi vimekuwa vikipanda kwa kasi na kufikia Juni 28 zaidi ya visa 80,000 vilikuwa vimeripotiwa.

Besigye pia alishutumu vikali serikali kwa kutoa Sh3,000 pekee kila mwezi kwa familia za jamii maskini wakati huu ambapo taifa hilo limefungwa.

Alisema kiasi hicho cha fedha ni kidogo mno huku akitoa wito kiongezwe hadi Sh8,000.

Waziri wa Jinsia, Leba na Maendeleo ya Kijamii, Bi Betty Amongi, mnamo Jumanne alisema kuwa maafisa kutoka Idara ya Kitaifa ya Takwimu pamoja na makarani wa miji mbalimbali, watasajili wananchi watakaonufaika na kitita cha Sh3,000 kinachotolewa na serikali kila mwezi.

Besigye pia anaitaka serikali iwalipie raia kodi za nyumba, kuwapa maji na kawi bila malipo na pia huduma zote za kimatibabu kwani kwa sasa wanapitia hali ngumu ya kiuchumi.

“Tulionya mapema kwamba uchumi na maisha ya raia yataathiriwa na janga hili, lakini serikali ilipuuza. Suluhu pekee ni kwa raia kutimiziwa mahitaji ya kimsingi hususan wakati huu wa masharti na kanuni kali za kudhibiti janga hili,’ akaeleza mwanasiasa huyo.

You can share this post!

BBI: LSK yadai ni rais alianzisha mageuzi

TAHARIRI: Tutahadhari shule zisifungwe kaunti 13