Habari Mseto

BETHA ACHIENG: Mkali wa video za kuvumisha nyimbo

February 19th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

PENYE nia pana njia, ndivyo wahenga walivyologa. Msemo huo ungali na mashiko sio haba miongoni mwa jamii kwa jumla.

Wengi walidhania angeibuka mchezaji wa kimataifa siku za usoni baada ya kutokea shupavu katika mchezo wa netiboli na pia mpira wa kikapu alipokuwa msomi kwenye shule ya upili ya Barchando Girls.

”Talanta yangu michezoni ilinisaidia pakubwa maana nilibahatika kufadhiliwa kupokea masomo ya sekondari baada ya kufanya mtihani wa darasa la nane,” anasema Betha Achieng na kuongeza kwamba kipindi hicho uigizaji aliuweka pembeni ingawa alianza kujituma katika masuala ya uigizaji tangu akisoma shule msingi.

Binti huyu ambaye ndiyo amefikisha miaka 22 ni mwanafunzi wa mwaka wa pili anaposomea taaluma ya uanahabari katika taasisi ya Aviation College Nairobi.

Kando na hayo, Betha anayejulikana kama Birocky amevalia kofia tofauti maana pia ni kati ya warembo (video vixen) ambao hufanya yao kusudi kuvutia watazamaji wa nyimbo za video pia ni mwigizaji anayeibukia.

”Nilitambua talanta yangu ya uigizaji tangu nikiwa mtoto ambapo hadi sasa ndiyo hufanya nipate riziki ya kila siku pia hugharamia mahitaji mengine ya kimaisha,” alisema na kuongeza kwamba licha ya umri wake anajivunia kuwa miongoni mwa waigizaji wanaolenga makuu siku sijazo.

Dada huyu anasema analenga kumiliki brandi yake ili kusaidia waigizaji ibuka hasa wanawake maana maprodusa wa kiume hupenda kuwakandamiza. Picha/ John Kimwere

Kipusa huyu anasema kando na kushiriki muvi nyingi tu ambazo zimefaulu kurushwa kupitia vituo tofauti vya televisheni hapa nchini anajivunia kushiriki nyimbo kadhaa kama video vixen.

Mrembo huyu anasema anafanya kazi ya muvi na kampuni ya Connie Kabbary Production inayopania kuzalisha muvi za viwango vya juu zitakazoonyeshwa hapa Kenya na pia nchini Nigeria.

”Mwezi Machi tunatarajia kusafiri Nigeria kushughulikia filamu zetu, baadaye tutarejea kufanya sehemu ya mwisho hapa nchini. Chini ya Connie Kabarry Production tunalenga kuzalisha muvi za levo ya kimataifa ili kutega soko la tasnia ya filamu na muvi hapa Kenya na Nigeria maana ni mradi tunaopania kushirikiana na mastaa wengi tu wa Nollywood.”

Kadhalika katika mpango mzima wanalenga kutangamana na wenzao hao ili kupata maarifa zaidi jinsi ya kufanya kazi bora za kupagawishwa watazamaji.

Katika uigizaji anasema anataka kujitahidi vilivyo kuhakikisha amefikia kiwango cha nyota wa Nigeria Mercy Johnson.

”Bila kujipigia debe hupenda kujifunza mengi na kazi za wenzangu ambapo mara nyingi hutazama muvi za mwigizaji huyo aliye kivutio cha wengi wetu,” alisema.

Kisura huyu tangia aanze uigizaji mwaka 2014 ameshiriki muvi fupi kama ‘Ghetto,’ TV Series ikiwamo ‘Mchungaji’ ‘The Real Househelps of Kawangware’ ambayo huonyeshwa kupitia KTN na  ‘Auntie Boss’ ya NTV.

Kama video vixen ameshiriki video za fataki kadhaa za waimbaji tofauti Afrika Mashariki kama Arrow bwoy ft Sudi Boy ‘Twende nalo,’ Kristof ‘Move it,’ King Kaka, Timmy Tdat ‘Magaldem’ na Alikiba wa Bongo Fleva ‘Kadogo,’ kati ya zingine.