Michezo

Betis watimua kocha baada ya mechi tatu pekee

June 25th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Real Betis kinachoshiriki Ligi Kuu ya Uhispania kimemfuta kazi kocha Joan ‘Rubi’ Francesc Ferrer baada ya mechi tatu pekee tangu kurejelewa kwa soka ya La Liga.

Kichapo cha 1-0 ambacho Betis walipokea kutoka kwa Athletic Bilbao mnamo Juni 20 kiliwasaza katika nafasi ya 14 jedwalini kwa alama nane zaidi nje ya mduara unaojumuisha vikosi vilivyopo katika hatari ya kushushwa ngazi mwishoni mwa msimu huu.

Zimesalia mechi nane pekee kwa kila kikosi kusakata katika kampeni za La Liga msimu huu.

Mkurugenzi wa spoti Alexis Trujillo ambaye alichezea Betis zaidi ya mechi 200, sasa atakuwa kocha mshikilizi hadi mwishoni mwa msimu huu.

Kibarua chake cha kwanza akidhibiti mikoba ya ukufunzi ni mechi itakayowakutanisha na Espanyol wanaokokota nanga mkiani mwa jedwali mnamo Alhamisi ya Juni 25, 2020.