Betis yapiga breki rekodi nzuri ya kocha Xavi kambini mwa Barcelona

Betis yapiga breki rekodi nzuri ya kocha Xavi kambini mwa Barcelona

Na MASHIRIKA

REKODI ya kutoshindwa kwa kocha Xavi Hernandez kambini mwa Barcelona ilipigwa breki kali na Real Betis waliopokeza miamba hao wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kichapo cha 1-0 mnamo Jumamosi ugani Camp Nou.

Juanmi alifungia Betis bao la pekee na la ushindi na akawapaisha hadi nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 30, tisa nyuma ya viongozi Real Madrid.

Xavi aliongoza waajiri wake kumenyana na Betis baada ya kushinda mechi mbili zilizotandazwa na Barcelona ligini pamoja na kuambulia sare tasa dhidi ya Benfica kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Kichapo kutoka kwa Betis sasa unawaweka Barcelona katika nafasi ya saba jedwalini kwa alama 23, sita nyuma ya mabingwa watetezi Atletico Madrid wanaofunga orodha ya nne-bora.

Barcelona walipoteza nafasi nyingi za kufunga kupitia kwa Philippe Coutinho na Ousmane Dembele. Masogora wa Xavi walihitaji ushindi katika mechi hiyo ili kupata motisha zaidi ya kuzamisha Bayern Munich katika mchuano wa kufa-kupona mnamo Disemba 7, 2021 ugani Allianz Arena, Ujerumani.

Mechi hiyo ilikuwa ya tatu mfululizo kwa Betis kushinda ligini na sasa wanajiandaa kumenyana na Celtic ya Scotland katika pambano la Europa League mnamo Disemba 9, 2021.

MATOKEO YA LA LIGA (Jumamosi):

Barcelona 0-1 Real Betis

Sociedad 0-2 Real Madrid

Sevilla 1-0 Villarreal

Atletico 1-2 Mallorca

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Shujaa yarejea nyumbani na majeraha

Polisi chonjo kukabili magenge msimu huu

T L