Bambika

Betty Kyallo afichua kuliendaje na Stivo Simple Boy

March 6th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

MFANYABIASHARA na mwanahabari Betty Mutei Kyallo amefunguka kuhusu mkutano wake wa hivi majuzi na rapa Stephen Otieno Adera almaarufu Stivo Simple Boy.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Betty amewakausha waliodhani mkutano huo ulikuwa na mwegemeo wa kimapenzi kati yao.

Akizungumza kwa njia ya simu, mwanahabari huyo alisema kilichowaleta pamoja ni mambo muhimu kujiboresha maishani, kinyume na madai ya baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Betty, hata hivyo, alidinda kufichua dili aliyodai “kuna kitu kwenye chungu motoni kikitokota”.

“Mkutano wetu kwa vyovyote vile hauhusishwi na mahusiano ya kimapenzi. Niliamua kutimiza ombi la Stivo Simple Boy kutaka sana tuoanane ana kwa ana,” akasema Betty akiangua kicheko kwa aliosuta wanaeneza uvumi usio na maana.

Alifafanua kwamba sababu kuu ya kukutana na mwanamuziki huyo ni kutokana na bidii na ari yake kushikilia uzi kutaka waonane.

Huku mastaa wengi ikiwa vigumu kukutana nao, Betty alisema yeye ni tofauti na kwamba habagui anayetamani kufanya mazungumzo naye ilimuradi tu yawe ni ya kuleta manufaa.

Msanii Stivo Simple Boy kwa muda mrefu amekuwa akitaka sana kukutana na mwanahabari huyo aliyevuma awali runingani, kiasi cha kuelezea hisia zake mitandaoni.

“Sikutaka kuonekana kuwa na pingamizi ya kukutana naye. Stivo ni msanii wa kujituma sana,” alisimulia Betty.

Baada ya mkutano wao uliofanyika katika mkahawa ambao Betty wakati wa mahojiano na Taifa Leo alikataa kufichua, mwanamuziki huyo alichapisha kwenye akaunti yake ya Instagram na Facebook picha zao wakiwa pamoja.

Mashabiki wao mitandaoni walieneza picha hizo mithili ya moto nyikani, kiasi cha kudai ndoano ya Stivo Simple Boy ilikuwa imenasa samaki baharini.

Mwanamuziki huyo akihojiwa na Trudy Kitui ambaye ni mtengenezaji wa maudhuo katika YouTube, alidai kwamba ilimgharimu zaidi ya Sh250,000 kufanya kikao na Betty.

“Nilitumia zaidi ya Sh250,000 kwa sababu Betty ni mrembo na gongigo zimeweza… mbona nisimshughulikie?” akauliza.

Alifichua kuwa mavazi aliyovalia, yalimgharimu Sh160,000.

“Kwanza koti, suruali ndefu na tai ni Sh125, 000. Viatu pekee vilimeza Sh40,000. Kwa ujumla, nilivyovalia thamani ilikuwa Sh165,000.”

Wachangiaji mitandaoni walitilia shaka madai ya kiwango cha fedha ambacho msanii huyo wa kibao tajika cha Vijana Tuache Mihadarati alitimia.

Betty hata hivyo alisema yeye alikuwa mwalikwa tu na hajui gharama iliyotumika.

Alikana tetesi kuwa yeye ndiye aligharimia bili hiyo.

“Sitazungumzia kuhusu kiwango cha pesa tulichotumia. Stivo Simple Boy alipanga kila kitu. Huenda amefanikiwa na ndio maana akagharimia alichogharimia. Tusiwe watu wa kudunisha wengine,” alisema.