Bambika

Betty Kyallo akanusha kuchumbiana na Ben 10

May 19th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

MWANAHABARI nguli wa runinga Betty Kyallo ambaye amerudi kupamba skrini majuzi, amekanusha uvumi unaosambazwa kuwa anachumbiana na mwanamume mdogo sana kwake kiumri.

Hii ni baada ya uvumi kuenea mtandaoni kwamba anakimbizana na dogo wa umri wa miaka 21 pekee.

Wakati wa mahojiano na Eric Omondi katika kipindi chake ‘This Friday With Betty’ katika runinga ya TV47 mnamo Ijumaa, alishangaa kufahamu uvumi huo ambao ni wa kupotosha kuhusu mahusiano yake na mpenziwe ambaye kwa sasa hajamtambulisha kwa ulimwengu.

Uvumi huo, ulitokea pindi tu Betty alipochapisha video kwenye kurasa za akaunti zake za mitandao ya kijamii, akionyesha zawadi alizopewa na mpenzi wake ambaye jina lake hajaliweka wazi.

“Alinipatia runinga ya inchi 77 na maua,” aliandika Betty kwenye ukurasa wake wa akaunti ya Instagram katika Siku ya Mama Duniani mnamo Mei 12, 2024.

Katika picha ya hivi majuzi iliyochochea uvumi huo, Betty alikuwa amechapisha picha ya miguu ya mpenziwe kwa viatu vizuri.

Wengi walidai kuwa wanamfahamu mtu aliyekuwa nyuma ya picha hiyo na kudai ni kijana wa umri wa miaka 21.

Katika kipindi chake cha Ijumaa, Betty alimkaribisha msanii Erico na kupiga naye stori ambapo alieleza kuhusu safari yake ya ucheshi kwa miaka 16 sasa.

Erico naye alimsomea Betty baadhi ya jumbe zilizotumwa kuhusu suala la mpenzi wake.

Alimtania akifichua kuwa pia “mimi na mpenzi wangu, pengo la umri ni miaka 20”.

Erico na mpenzi wake wana mtoto wa kike.

“Tulisoma na huyo mvulana wa Machakos Boys miaka miwili iliyopita,” shabiki mmoja alisema kwenye ujumbe ambao Erico alimsomea Betty.

Betty alisema madai hayo yalimshtua lakini akapuuzilia mbali akisema ni uongo yeye hajafuga kijana Ben 10.

“Taarifa mliyoipata ilikuwa si sawa, miaka 21! Ni uongo,” alisema Betty.

Hata hivyo aliendelea kutania jinsi wazee wanavyochoshwa na kuonyesha upendo kwa kuwa wanashikiliwa na familia na masuala mengine.

Mnamo Mei 10, 2024, Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Kalerwa Salasya alikuwa mgeni wa Betty studioni wakati kipindi chake kilizinduliwa rasmi.

Bw Salasya alimpelekea Betty maua kumkaribisha rasmi.