Habari Mseto

Betty Kyallo alaumu mazingira magumu ya biashara kwa duka lake kunadiwa

April 8th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

MFANYABIASHARA Betty Kyalo, amefichua sababu za kushindwa kulipa kodi ya duka analomiliki, Flair by Betty salon katika mtaa mmoja wa kifahari Kaunti ya Nairobi.

Kulingana na mjasirimali huyu ambaye pia amewahi kuhudumu kama mtangazaji wa runinga, hali ngumu ya biashara ndiyo imechochea kulemewa kulipa deni la Sh1.5 milioni analodaiwa.

Betty amesema mazingira magumu ya biashara nchini ndiyo chanzo cha changamoto anazopitia.

Alidai kutokuwepo kwa maelewano kati yake na mmiliki wa duka analohudumu kupunguza kodi, ndiyo sababu ya mrundiko wa pesa anazodaiwa.

“Imekuwa vigumu sana kuendeleza biashara hapa nchini. Nilifanya mazungumzo na mmiliki wa nyumba apunguze kodi, ambayo imekuwa mzigo mzito kwa biashara. Biashara hazifanyi vyema kutokana na uchumi kudorora,” alielezea.

Taarifa ya mtangazaji huyo kulemewa kulipa kodi, ilifichuka Jumatatu, Aprili 8, 2024 kupitia tangazo la vifaa vyake kunadiwa.

Aidha, lilichapishwa kwenye nakala ya gazeti moja nchini.

Betyy alisema hatua iliyochukuliwa na mmiliki wa duka, kupiga mali yake ya kazi kunampa amani.

Alisema ataweza kujilipa kodi anayomdai.

“Inaumiza kuona vitu hivyo vikiuzwa. Lakini pia, nafurahia nikijua nitalala na amani na utulivu,” alisema Betty Kyallo.

Mama huyo wa mtoto mmoja aliambia Taifa Dijitalilicha ya vifaa vyake vya kazi kunadiwa, alifanikiwa kufungua duka lingine katika mtaa wa kifahari wa Upper Hill miezi miwili iliyopita.

“Kila biashara huwa na changamoto zake. Najua nitaweza kuimarika zaidi baada ya kufungua duka lingine ambalo linatoa huduma kama za hapo awali na wateja wangu watafurahia,” aliongeza.

Mfanyabiashara huyo, pia, alitumia fursa ya mahojiano na Taifa Dijitali kushukuru Wakenya waliomfariji na kumtia motisha kwa biashara yake kufungwa ghafla.

Kwenye notisi iliyochapishwa kwenye gazeti, wapiga mnada kutoka kampuni ya Keysian walisema vifaa vyote vilivyo kwenye duka la mfanyabiashara huyo, vitauziwa umma mnamo Jumatano, Aprili 17, 2024, baada ya mmiliki wa nyumba kuwasilisha kesi hiyo.

Uuzaji huo umeratibiwa kufanyika kwenye duka la Leakey’s Storage Limited, katika barabara ya Lung-Lunga Jijini Nairobi.

Duka hilo ambalo lilikuwa likitoa huduma za kunyoa nywele na ususi, lilifunguliwa 2020.

Wateja wamekuwa wakitozwa ada ya Sh 1,500 hadi Sh 5,000 kulingana na mtindo.

Pia, lilijumuisha biashara ya ukandaji mwili – massage.

Mwaka uliopita, 2023, Betty Kyallo alifungua tawi lingine mjini Meru, na kusherehekea kwa kufanya vizuri katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.