Habari Mseto

Betty Maina ashauri vijana wakatae kuingizwa boksi na wazee

January 29th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

MBUNGE Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Murang’a Betty Maina amewataka wenyeji wakome mtindo ambao unapata umaarufu, wa vijana wa kiume kupendana na wanawake wa umri wa shangazi zao huku wale wa kike wakiingizwa boksi na wazee.

Mwanamume mzee anayewinda wanawake wadogo kiumri huitwa ‘mubaba’ katika lugha ya mtaa. Naye mwanamke mkubwa kiumri anayewinda vijana wa kiume almaarufu Ben 10, huitwa ‘mumama’.

Bi Maina amlisema mtindo wa wanawake wakubwa sana kiumri kuwanyemelea vijana wa kiume wadogo wao unapata umaarufu huku nao wazee wakiwawinda wanawake walio wadogo kiumri na ambao hata ni wa rika la wajukuu wao.

“Ushauri wangu ni kwa wasichana na wavulana wetu wajiingize tu kwa mapenzi na walio wa rika lao,” akasema Bi Maina.

Alisema kwamba mapenzi ya kuweka pesa na zawadi mbele huwa hayana maana kwa sababu hayawi ya dhati.

Aidha, aliwataka wanawake wawe wanafanya utafiti kuhusu wanaume wanaopendana nao ili kujiepusha na matukio ya dhuluma na mauaji.

“Chukueni tahadhari. Acheni haraka,” akasema, huku akionya kwamba suala la mauaji yanayowalenga wanawake linafanyiwa utani.

[email protected]