BETWAY CUP: Congo Boys wangali wataka kucheza na Gor uwanja wao wa Serani

BETWAY CUP: Congo Boys wangali wataka kucheza na Gor uwanja wao wa Serani

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

CONGO Boys FC inaonelea fahari kuu ikiwa timu kubwa mbili za hapa nchini, Gor Mahia na AFC Leopards zitacheza mechi kwenye uwanja wao wa Serani Sports, mjini Mombasa.

Hayo yalisemwa na Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) wa Congo Boys FC, Ali Said amesema wanaliomba Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) litayarishe pambano lao la Raundi ya timu 16 la Betway Cup dhidi ya Gor Mahia FC katika uwanja huo wao wa Serani Sports.

“Mechi hii sisi ndio timu ya nyumbani na kwa kuwa tuna uwanja mzuri wenye sifa zote za kuandaa mechi kubwa, tungependelea mchezo wet una Gor ufanyika hapo badala ya kupangiwa kuchezwa uwanja wa Mbaraki Sports Club,” akasema Said.

Alisema kuthibitishwa kuwa uwanja wao ni mzuri na unaostahili kwa mechi hiyo na Gor ni kwamba ndio unaotumiwa kwa mec hi za Supaligi ya Taifa na Modern Coast Rangers na timu yake ya Congo inayoshiriki kwenye Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza.

“Kwa kuwa mechi kubwa za supaligi ya taifa pamoja na ligi ya taifa daraja la kwanza zinachezwa hapo Serani Sports ambapo kuna ulinzi wa kutosha, tunaomba FKF itukubalie ombi letu mechi dhidi ya Gor ichezwe hapo maana tutajivunia kwa uwanja kutumiwa na timu kubwa hiyo,” akasema.

Afisa huyo alitoa ombi hilo katika uwanja wa Mbaraki Sports Club ambapo timu yake ilicheza na timu ya Ligi Kuu ya FKF, Bandari FC katika mchezo wa kujipima nguvu ambapo Bandari iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, mabao yote yakitingwa kipindi cha pili.

Congo Boys ilijikaza na kuweza kuhakikisha wanapumzika wakiwa sare tasa na wapinzani wao hao wa Bandari. Lakini kipindi cha pili, Bandari iliyochezesha wanasoka kadhaa chipukizi, ilijipatia mabao mawili wafungaji wakiwa John Mwita dakika ya 56 na Dennis Katana dakika ya 71.

Naibu kocha wa Congo Boys, Nassir Kassim alisema kuwa wamecheza mechi hiyo kwa ajili ya kuuzoea ikiwa watacheza mchezo wao wa Betway Cup na Gor katika uwanja huo. “Nawapongeza vijana wangu kwa jinsi walivyocheza vizuri ingawa tulishindwa,” akasema Kassim.

You can share this post!

KAMAU: Nani akomboe Kenya kutokana na ufisadi?

BI TAIFA MACHI 1, 2021