Michezo

Betway Cup raundi ya 16 kugaragazwa wikendi kote nchini

March 13th, 2020 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

LIGI Kuu ya Kenya (KPL) itapumzika wikendi hii kupisha michuano Betway Cup raundi ya 16 Bora itakayoshuhudiwa katika viwanja mbali mbali kote nchini.

Katika michuano hiyo ya muondaono, kesho Jumamosi kuanzia saa saba itakuwa zamu ya Wazito FC na Kenya Commercial Bank (KCB) katika uwanja wa Afraha Nakuru, kabla ya Gor Mahia kuingia uwanjani humo baadaye kucheza na Posta Rangers.

Kwingineko hiyo kesho Jumamosi, Bandari watakuwa wenyeji wa Sofapaka kuanzia saa kumi ugani Mbaraki Sports Club, Mombasa.

Jumapili, Ulinzi Stars watakuwa wenyeji wa Migori Youth ugani Afraha Nakuru kuanzia saa saba, kabla ya AFC Leopards kujibwaga uwanjani humo kukabiliana na Ushuru FC kuanzia saa tisa unusu.

Timu ya Fortune Sacco inayoshiriki Supa Ligi ya Kenya (NSL) itakuwa nyumbani uwanjani Kianyaga kesho Jumamosi kucheza na Bidco United kuanzia saa tisa.

Mjini Kisumu siku ya Jumapili, mashabiki watamiminika Moi Stadium kushuhudia pambano kati ya wenyeji Kisumu All Stars na Keroka Technical University, huku Kariobangi Sharks wakipepetana na FC Talanta ugani MISC, Kasarani.

Bingwa wa Betway Cup atapokea Sh2 milioni mbali na tiketi ya kuwakilisha Kenya katika mashindano ya CAF Confederations Cup, msimu ujao.

Akizungumza kuhusu mechi yao dhidi ya Ushuru, kocha Anthony Kimani wa AFC Leopards alisema atahakikisha kwamba vijana wake wamepata ushindi na kusonga mbele katika michuano hiyo ya muondoano.

Kimani alisema kwamba ana hakika kuwa vijana wake watapata ushindi baada ya kufanyia marekebisho makosa yaliyotokea katika mechi yao dhidi ya Gor Mahia ambapo walipoteza nafasi nyingi na kushindwa 1-0.

“Tumejiandaa vyema kwa mechi ya Jumapili. Wachezaji wako fiti na matarajio yetu ya kutwaa ubingwa wa msimu huu ni makubwa hasa baada ya matumaini ya kushinda ubingwa wa KPL kuendelea kudidimia,” aliongeza.

Hata hivyo, Kimani atapanga kikosi chake bila nyota Mervin Wabwire anayeuguza jeraha lakini atakuwa na mastaa wake wote wa kutegemewa.

Katika uwanja uo huo, licha ya ubora walionao na kufanya vizuri katika ligi kuu ya KPL, Gor Mahia wanatarajiwa kukumbwa na kibarua kigumu mbele ya vijana wa Posta Rangers katika mechi nyingine itakayochezwa kesho.

Mechi hii ionatarajiwa kuwa ngumu kutokana na timu hizi mbili kucheza mpira wa nguvu na kasi, hasa ikizingatiwa kuwa katika mechi ya mkondo wa kwanza ya ligi kuu iliyochezewa Narok, timu hizo zilitoka sare ya 1-1 lakini baada ya K’Ogalo kutolewa jasho.