Michezo

Beyern kutawazwa mabingwa wakiilima Bremen

June 15th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

BAYERN Munich watakuwa wageni wa Werder Bremen uwanjani Weser mnamo Juni 16, 2020 katika mchuano ambao wana ulazima wa kusajili ushindi ili kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa msimu wa nane mfululizo.

Kwa upande wao, Bremen wanafahamu kuwa kushindwa kwao kutadidimiza zaidi matumaini yao finyu ya kutoshushwa ngazi mwishoni kampeni za muhula huu.

Licha ya kusajili ushindi mnono wa 5-1 dhidi ya limbukeni Paderborn mnamo Juni 11, Bremen wanashikilia nafasi ya 17 jedwalini kwa alama 28 sawa na Dusseldorf ambao watakuwa wageni wa RB Leipzig mnamo Jumatano ya Juni 17. Ni pengo la alama nane pekee ndilo linalotamalaki kati ya Bremen na Paderborn wanaovuta mkia.

Japo Bayern hawakuwa katika ubora wao wa kawaida walipovaana na Borussia Monchengladbach mnamo Juni 13, ushindi wao wa 2-1 katika mechi hiyo uliwanusisha ufalme wa Bundesliga kwa mara nyingine.

Mabao ya Bayern katika gozi hilo lililosakatiwa ugani Allianz Arena, yalifumwa wavuni na Leon Goretzka na chipukizi Joshua Zirkzee.

Mbali na kufukuzia ubingwa wa Bundesliga chini ya kocha mpya Hansi Flick, Bayern wangali wanawania ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na tayari wametinga nusu-fainali ya German Cup itakayowakutanisha na Bayer Leverkusen mwishoni mwa Juni 2020.

Ushindi kwa Bayern dhidi ya Bremen utakuwa wao wa 12 mfululizo katika kampeni za Bundesliga. Miamba hao wanatazamia kuwakaribisha kikosini vigogo Thomas Muller na Robert Lewandowski ambao kwa pamoja, wamefungia Bayern jumla ya mabao 64 kufikia sasa msimu huu.

Wawili hao walikosa mechi dhidi ya M’gladbach kutokana na marufuku yaliyochangiwa na wingi wa kadi za manjano. Kurejea kwao kutawaweka benchi wachezaji Michael Cuisance na Zirkzee huku Alphonso Davies na Kingsley Coman wakitarajiwa pia kutwaa nafasi za Lucas Hernandez na Ivan Perisic katika kikosi cha kwanza.