Kimataifa

Bi harusi aokota chupa 800,000 kuweka rekodi

November 22nd, 2018 1 min read

MASHIRIKA Na GEOFFREY ANENE

BI harusi mmoja kutoka Australia ameamua kuokota maelfu ya chupa za plastiki ili aweze kutimiza ndoto yake ya kuwa na harusi kubwa ya Sh6,025,201 nchini Vanuatu.

Vyombo vya habari nchini Australia vimeripoti kwamba Leonie Starr alisema katika ukurasa wake wa Facebook kwamba lengo lake ni kukusanya zaidi ya chupa 800,000 katika kipindi cha mwaka mmoja ujao.

Kila chupa inayoweza kutumiwa tena itamletea Senti 10.

“Kupitia usaidizi wa kila mtu, nadhani tunaweza kufanikiwa! Kichuna huyo mwenye umri wa miaka 28 alichapisha katika ukurasa wake. Starr na bwana harusi Matthew Porter wanataka kuwa na harusi ya kukata na shoka katika kisiwa cha Vanuatu, lakini itawagharimu karibu dola za Australia 81, 000 (Sh 6,025,201 za Kenya).

Kisiwa hiki kinapatikana kilomita 1,750 Kaskazini mwa Australia katika Bahari ya Pacific. Familia ya Starr na marafiki zake sasa wanamwasilishia chupa zilizotupwa.

“Mwanzoni, walicheka. Waliona kama ni wazo la kipuzi, wakidhani halitawahi kufanyika,” aliambia Shirika la Utangazaji la Australia (ABC). “Hata hivyo, kila mtu amechangamkia wazo hili. Hata wale ambao hawapendi kukusanya chupa zilizotupwa zinazoweza kutumika tena. Watu wengi wamezamia shughuli hii, inafurahisha.”

Starr amekuwa akifanya usafi huo wa kukusanya chupa katika mabustani na fukwe za bahari na anauliza watu kuchangia. Wapenzi hawa wanapanga kufunga pingu za maisha mwezi Machi mwaka 2020.