Habari Mseto

Bi Kenyatta ashauriana na Malkia Mathilde wa Ubelgiji

June 27th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA na PSCU

BI Margaret Kenyatta ambaye ni mkewe Rais Uhuru Kenyatta, Jumatano alifanya mashauriano na Malkia Mathilde wa Ubelgiji ambaye alimtembelea katika Ikulu ya Nairobi.

Mama wa Taifa na Malkia Mathilde walijadili mbinu za kuongeza upatikanaji wa elimu na huduma za afya hususan kwa zile jamii ambazo zinakabiliwa na changamoto.

Bi Kenyatta alimfahamisha Malkia wa Ubelgiji kuhusu ruwaza yake ya Beyond Zero kwa ajili ya afya bora nchini Kenya akisema mpango huo umesaidia kusambaza kliniki tamba 52 zenye vifaa kamili kote nchini kama sehemu ya juhudi za pamoja zinazoendelea kupeleka huduma za afya karibu na wananchi.

“Sasa tumerejelea mpango wa nyanjani kupitia safari za kupeleka huduma za afya mashinani za Shirika la Beyond Zero ambapo watu hupokea huduma za matibabu bila malipo dhidi ya maradhi mbali mbali,” akamfahamisha Malkia huyo.

Bi Kenyatta alisema anapigia debe juhudi za kuhakikisha mama wajawazito wananufaika na huduma zaidi za afya kutoka kwa wahudumu wa afya wenye maarifa ili kukabili visa vya nasuri.

Kuhusu elimu, Mama wa taifa Margaret Kenyatta alimfahamisha Malkia huyo kuhusu mpango wa kuwatuza wanafaunzi chini ya mpango ujulikanao kama, PURES, ambao ni mradi wa kipekee wa kuwamotisha wanafunzi kote nchini watie bidii masomoni.

Mradi huo ulioanzishwa na Rais Uhuru Kenyatta pia unalenga kuwapa wanafunzi hao maadili ya uzalendo, nidhamu na mwelekeo.

Malkia Mathilde ambaye yuko nchini kwa ziara ya siku tatu ya majukumu ya shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu ya Watoto, (UNICEF) kutoa uhamasisho kuhusu matatizo ya elimu na watoto wanaoishi katika hali ngumu, alimuarifu Bi Kenyatta kuhusu ziara yake huko Kakuma kaunti ya Turkana ambapo alitembelea kambi ya wakimbizi ya Kakuma.

Mgeni azuru Kalobeyei

Vilevile, mgeni huyo alizuru kituo cha elimu ya chekechea cha Kalobeyei pamoja na shule ya msingi ya Kalobeyei zilizojengwa na shirika la UNICEF na lile lile la wakimbizi la UNHCR.

Malkia huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Heshima wa shirika la Unicef nchini Ubelgiji vilevile alisema alizuru Kituo cha Amref cha Ustawi wa Watoto kilichoko eneo la Dagoretti na makazi ya mabanda ya Korogocho, Nairobi ambako alikumbana waziwazi na mahitaji ya kielimu ya watoto kutoka famila za kipato cha chini.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mwakilishi wa UNICEF hapa nchini Bi Maniza Zaman alimpongeza Bi Kenyatta kwa kuongoza harakati za kuboresha afya ya watoto na akina mama hapa nchini.

Bi Zaman alisema shirika lake linatafuta namna ya kushirikiana kikazi na shirika la Beyond Zero akisema afya na elimu ni masuala yanayotangamana.