Makala

BIASHARA MASHINANI: Ajira iliadimika, akamakinika katika kukuza kitunguu saumu

August 1st, 2019 2 min read

Na PETER CHANGTOEK

BAADA ya kuhitimu katika chuo kikuu cha JKUAT na kupata stashahada katika masuala ya usimamizi wa biashara mnamo mwaka 2015, Lawrence Rotich alianza kusaka ajira lakini mambo yakamwendea segemnege.

Hapo ndipo alipoamua kujitosa kwa shughuli za zaraa, hususan ukuzaji wa vitunguu saumu.

“Nimekuwa nikitamani kujiajiri mwenyewe, na kilimo ndicho kimenipa nafasi nzuri,” asema.

Mwanzoni, alianza kujishughulisha na ukuzaji wa viazi vyeupe na vitunguu saumu, kwa kutumia mtaji wa Sh60,000.

“Jirani yangu mmoja aliyekuwa amekuza vitunguu saumu kwa muda mrefu na kufanikiwa alinijuza kuwa vitunguu saumu ni bora,’’ asema Rotich.

Kwa wakati huu, mkulima huyo ana mimea ya vitunguu saumu katika shamba ekari moja katika eneo la Segemian, kaunti ya Narok.

“Mwanzoni, nilivipanda vitunguu saumu kilo 50 katika shamba nusu ekari, nilivyovinunua kutoka kwa jirani yangu mmoja aliyekuwa amevikuza kwa miaka mingi,” afichua mkulima huyo, ambaye huvikuza vitunguu saumu aina ya hardneck.

Rotich, ambaye huvikuza vitunguu saumu mara mbili kwa mwaka mmoja, anadokeza kwamba vitunguu saumu huchukua muda wa miezi minne hadi sita ili kukomaa, ikitegemea hali ya anga.

Anaeleza jinsi anavyolitayarisha shamba kabla hajavipanda vitunguu saumu: “Kabla sijapanda, mimi huchanganya mbolea za kiasili pamoja na mchanga ili kupata mazao bora. Mimi hulitumia jembe kuitengeneza mistari ya kupandia kwa kuiacha nafasi ya sentimita 30.’’

Baada ya kuvipanda, mkulima huyo pia huyatandaza matandazo ili kuzikinga mbegu zinazoota. “Mbegu zinapoanza kuchipuka, matandazo hayo hutolewa,” asema akiongeza kuwa wakati uo huo, magugu hung’olewang’olewa hadi wakati vitunguu saumu vitakapokomaa.

Japo vitunguu vyake vimewahi kuathiriwa na baadhi ya magonjwa kama vile ugonjwa wa kunyauka kwa majani, changamoto kuu ambayo mkulima huyo anasema humkumba sana ni maotea au magugu yanayoota shambani.

“Ni sharti magugu yang’olewe kila wakati. Mvua zimekuwa zikinyesha kwa wingi, jambo linaloyafanya magugu hayo yaote. Aidha, kupata soko ni changamoto,” asema mkulima huyo, mwenye umri wa miaka 28.

Yeye huyauza mazao yake kwa wafanyabiashara wadogo wadogo na wakulima wanaovitumia vitunguu hivyo kuwa mbegu. Yeye huviuza vitunguu vyake kwa Sh150-Sh200 kwa kilo moja.

 

Lawrence Rotich aonyesha vitunguu saumu anavyokuza katika eneo la Segemian, Kaunti ya Narok. Picha/ Peter Changtoek

Anaongeza kuwa hutumia mbolea aina ya DAP wakati anapozipanda mbegu zake.

Rotich anafichua kuwa hulitumia shamba lake kukiendesha kilimo hicho. Anadokeza kuwa ana shamba ekari kumi, lakini sehemu kubwa ya shamba hilo hutumika kwa shughuli ya ufugaji wa ng’ombe.

Kwa mujibu wa mkulima huyo, ukuzaji wa vitunguu saumu una tija. “Mie hupata kati ya Sh200,000 na Sh300,000 kwa msimu mmoja. Hii ni kwa sababu ya kukosa soko bora. Naamini kuwa ninaweza kupata pesa nyingi zaidi endapo nitapata soko bora. Ninaazimia kujitosa katika uzalishaji wa vitunguu saumu kwa wingi iwapo nitapata soko la kutegemewa,” asema Rotich, ambaye ni baba wa mtoto mmoja.

Mkulima huyo anasema kuwa ni muhimu kwa mkulima kulitafuta soko kwanza, la sivyo mazao mengi yataharibika.

Anawashauri vijana kujishughulisha na shughuli za kilimo badala ya kusubiri kupata ajira za afisini.

Pia, anawashauri wale wanaonuia kujitosa kwa shughuli ya ukuzaji wa vitunguu saumu kufanya utafiti kwanza kuhusu aina ya vitunguu ambavyo hukua vyema katika maeneo yao.

“Ni muhimu kutafuta soko kwanza kabla hujavuna. Ukuzaji wa vitunguu saumu una faida iwapo utaendeshwa ipasavyo,’’ ashauri mkulima huyo, ambaye mbali na kujishughulisha na uzalishaji wa vitunguu saumu, hujishughulisha pia na uzalishaji wa mahindi na ufugaji wa ng’ombe.