BIASHARA MASHINANI: Lishe mbovu nusura ifagie sungura wake; akaokoa hali

BIASHARA MASHINANI: Lishe mbovu nusura ifagie sungura wake; akaokoa hali

Na PETER CHANGTOEK

MAUREEN Wanyaga, 29, aliwapoteza wazazi wake mnamo 2005 kwa ajali ya barabarani, walipokuwa wakienda kumtafutia shule ya upili, ambayo angejiunga nayo, baada ya kukamilisha masomo ya shule ya msingi.

Hata hivyo, hakukata tamaa asilani, bali aliendelea na masomo yake hadi akafuzu na kupata shahada ya uzamili (Master’s degree). Licha ya kuwa na shahada hiyo, alitafuta kazi pasi na mafanikio, ndiposa akajitosa katika ufugaji wa sungura.

Kwa sasa, ana sungura 850. Alikuwa na 1,000, lakini wengine walikufa, kwa sababu ya kuwalisha kwa lishe za madukani, ambazo anaamini kwamba zilikuwa na sumu. Hata hivyo, hajatazama nyuma na anazidi kuchuma kutokana na kilimo hicho.

“Nilizaliwa jijini Nairobi, lakini nilikuja hapa Nyeri 2015 kwa sababu ya ufugaji wa sungura,” asema Wanyaga, ambaye ana shahada katika masuala ya biashara (BCom) na shahada ya uzamili kwa masuala ya usimamizi wa biashara, kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT).

Anadokeza kuwa, alipokuwa katika chuo kikuu, alikuwa akiviuza vitabu na pia alikuwa na pikipiki ambayo ilikuwa ikimpa fedha ambazo zilikuwa zikimsaidia. Kutokana na shughuli hizo, aliweka akiba ya Sh50,000, pesa taslimu, ambazo alizitumia kuanzisha shughuli hiyo ya ufugaji wa sungura.

“Tulipowapoteza wazazi wetu, shangazi na mjomba wakatuchukua, na tulikuwa tukila nyama ya sungura kila wakati, na baadaye, nikawapenda sungura na kuanza kuwafuga baada ya kukamilisha masomo ya chuo kikuu,” asema mkulima huyo.

Anaongeza kuwa, aliamua kujitosa katika ufugaji wa sungura kwa sababu si watu wengi waliokuwa wakiendeleza kilimo hicho kwa wakati huo.

Anasema kuwa, hapo awali, alikuwa akiwalisha sungura wake kwa lishe alizokuwa akizinunua kutoka kwa kampuni ya Unga Farm Care, lakini Septemba, mwaka jana, aliacha kuzinunua lishe hizo kwa sababu sungura wake wengi walikufa baada ya kuwalisha.

“Lishe zao zilikuwa na sumu, na ziliwaua sungura kote nchini Kenya, na hata shirika la KEBS likatwaa leseni yao ya kutengeneza lishe za sungura. Kabla lishe hizo hazijawaua sungura wangu, nilikuwa na 1,000, lakini kwa sasa nimebaki na 850,” asema.

Wanyaga anasema kwamba, alianzisha shughuli hiyo ya ufugaji kwa kuwafuga sungura wanne wa kike na mmoja wa kiume, aliowanunua kutoka kwa taasisi moja ya serikali iliyoko mjini Ngong.

Aliwanunua kwa Sh3,000 kila mmoja.

Mkulima huyo anafichua kuwa, hapo awali, alikuwa na changamoto ya kupata soko la kuwauzia sungura wake, lakini kwa sasa, hana tatizo la kuwapata wateja. Mara nyingi, yeye hutangaza biashara yake kwa mitandao ya kijamii.

Anasema kuwa, ni jambo aula kuwa mtu wa kuaminika kwa wateja kila wakati, ili kutowapoteza.

“Kuwa mwaminifu kwa wateja, na watarudi tena kununua na kuwaambia wengine. Pia, uwajali hata baada ya kuwanunua,” asema Wanyaga, akiongeza kuwa, huwauza sungura wake kote nchini.

Humwuza mmoja mwenye umri wa miezi mitatu kwa Sh1,500 na wale waliokomaa kwa Sh3,000 kila mmoja.

Mkulima huyo huwafuga sungura wa aina tofauti tofauti, mathalan: New Zealand, California White, Dutch, Flemish Giant, Earlope, Angora.

Anaongeza kuwa, hapo mbeleni, alikuwa akiuza nyama ya sungura, lakini akasimamishwa na shirika la kukadiria ubora wa bidhaa nchini (Kenya Bureau of Standards).

“Usiseme hakuna kazi, anza kwa kidogo ulicho nacho,” ashauri.

Natumia shamba 1/8 ekari. Lina vibanda 500 vya kisasa. Ninapanga kuongeza idadi ya sungura kutoka 850 hadi 5,000, na kuanza kujitengenezea lishe, na kuuza nje ya nchi,” afichua Wanyaga.

You can share this post!

AKILIMALI: Ni mashine ya kisasa ya kuchuma chai, lakini...

AKILIMALI: Aamini unyunyiziaji huu utaifanya Kenya kupiku...