Makala

BIASHARA MASHINANI: Malengo yake ni kugeuza kijiji kuwa kitovu cha maziwa

July 18th, 2019 3 min read

Na PHYLLIS MUSASIA

KIJIJI cha Surungai katika eneobunge la Cherang’any, Kaunti ya Trans-Nzoia hakina umaarufu, na kila kitajwapo, wengi watakuambia kwamba jina hilo ni geni.

Lakini kwa ukakamavu wake Bw Allan Mwangi ambaye ni mwalimu mustaafu, ana matumaini ya kubadilisha kijiji hicho kwa kufanya kilimo tofauti na kile cha mahindi ambacho ndicho kitega uchumi kwa wakazi wengi wa hapa.

Kazi yake kuu ni kufuga ng’ombe wa maziwa.

Bw Mwangi amekuwa kwenye kazi hii tangu miaka ya tisini na anasema kwamba, siri ni ukakamavu, uvumilivu na kuwa na malengo dhabiti na kuyaafikia.

Ndama katika shamba la Allan Mwangi. Picha/ Phyllis Musasia

Alianza kwa kufuga ng’ombe wawili tu wa aina ya Friesian na ng’ombe mmoja wa kienyeji.

Angepata lita tano pekee za maziwa kutoka kwa ng’ombe hao lakini hilo halikumfisha moyo bali ikawa ni ufunuo mpya kwake kutaka kufuga ng’ombe wengi ili kuongeza idadi ya lita alizotarajia kupata kwa siku.

“Katika utafiti wa hapa na pale, nilipata wazo tafauti na baada ya muda fulani niliamua kubadilisha ng’ombe hao wawili niliokuwa nao na kununua ng’ombe wengine aina moja ya Ayrshire,” akasema Bw Mwangi na kuwasifia sana ng’ombe wake.

Alieleza kuwa aina ya ng’ombe wa Ayrshire ni imara na kwamba hawapatwi na matatizo ya magonjwa kiholela.

“Wana uwezo wa kudhibiti aina yoyote ya magonjwa na kuishi katika aina yoyote ile ya mazingira,” akaongeza.

Asema kuwa maziwa wanayotoa ng’ombe wa aina ya Ayrshire ni ya kiwango cha juu cha mafuta ikilinganishwa na maziwa ya ng’ombe wengine.

Kwa jumla, mkulima huyo sugu ana jumla ya ng’ombe sita na ndama saba ambao wamemwezesha kuwalipia wanawe karo ya shule, bili kama vile za maji, umeme na kuwekeza bima ya matibabu kwa familia yake ya watu sita.

“Tangu nilipostaafu sijawa na shida ya hela. Nimejikakamua kuona ya kwamba kilimo hiki kinasalia imara licha ya changamoto za hapa na pale,” akasema baba wa watoto watano.

Kwa siku moja Bw Mwangi alisema kuwa ng’ombe wake wanampa jumla ya lita 86 za maziwa huku ng’ombe mmoja aliyemnunua kutoka Finland akimwezesha kupata lita 40 asubuhi na adhuhuri.

“Maziwa haya mimi huuza kwenye maduka ya maziwa hapa Cherang’any ambapo lita moja huwa kwa Sh35,” akaeleza.

Ili kuzalisha ng’ombe wake, alisema yeye huagiza shahawa kutoka nchi ya Canada ambayo iko na ng’ombe wazuri wa kiume ili kupata ndama wenye afya bora.

“Huwa nahakikisha kuwa natumia mbinu za kisasa za kuzalisha ng’ombe wangu na kuhusisha wataalamu wa masuala ya mifugo katika kila kiwago,” akasema Bw Mwangi.

Ng’ombe mmoja wa aina ya Ayrshire, alisema, huuzwa kwa kwa kati ya Sh150, 000 na Sh200, 000 kwa wale ambao hawajafikia kiwango cha kuzaa.

Kwenye ekari mbili za shamba lake, mkulima huyu ameweza kupanda aina mbalimbali ya chakula cha ng’ombe wake ikiwemo nyasi za Boma Rhodes.

Anatazamia kuogeza kiwango hicho cha chakula kwa zaidi ya shamba ukubwa wa ekari saba.

“Kiasi cha chakula wanachokula ng’ombe huwezi kulinganisha na binadamu. Hawa wanakula usiku na mchana na ndio maana ninatazamia kuongeza chakula zaidi hadi kufikia ekari saba za shamba langu,” akasema Bw Mwangi huku akiongeza kuwa idadi ya ng’ombe hao huongezeka kwa kasi mno.

Mahindi

Chakula kingine ambacho kinakua shambani mwake ni mahindi ya ‘yanga’ almaarufu yellow maize.

Anasema mahindi hayo yana kiwango cha juu cha madini ambayo husaidia ng’ombe kutoa maziwa mengi na yenye uzito.

“Mimea mingine kama vile sunflower na maharangwe ya soya pia husaidia sana mifugo kupata protini zinazohitajika mwilini. Wakati huo huo, mimea hiyo husaidia mchanga kwa kufungua mashimo ya mchanga na kuvuta oksijen, hali ambayo ni bora kwa upanzi,” akaeleza Bw Mwangi.

Alisema ili kuhakikisha kwamba viini vya sumu ya mbolea na kemikali anazotumia kukuza mimea hiyo haifiki kwenye maziwa, yeye hutumia dawa ya kusawazisha aina yoyote ya kemikali kwenye mwili wa mfugo.

Kilimo hiki kimemwezesha kuungana na watu wegine ambao wako na maono sawia na yake na kumsaidia kujiunga na vikundi mbali mbali.

Kunacho kikundi kimoja ambacho Bw Mwangi alisema kimemwezesha kupiga jeki kilimo chake kwani wakulima huwezeshwa kupata mikopo ya kuwasaidia kuendeleza kazi yao.

Mwaka uliopita, wakulima hao waliwezeshwa kupata Sh700, 000 pesa ambazo alisema hutumika kwa madawa na chakula cha mifugo hao.

Kwenye shamba lake, Bw Mwangi ameweza kuajiri watu wanne ambao hushughulikia ng’ombe hao mbali na kujihusisha na kazi nyinginezo.