Makala

BIASHARA MIJINI: Wauzaji vinyago wajikakamua licha ya kupungua kwa watalii

July 25th, 2019 3 min read

Na SAMUEL BAYA na KEVIN ROTICH

NI saa sita mchana na katika barabara ya Kenyatta katikati wa mji wa Nakuru, shughuli za kutafuta riziki zimenoga.

Jambo moja linalotuvutia ni msururu wa vibanda vya kuuza vinyago ambavyo vinapatikana kwa wingi hapa.

Ari yetu ya kutaka kujua mengi kuhusu biashara hii inatufikisha katika kibanda cha James Shiundu. Ni mwaka wa sita tangu aingilie kazi hii ya kuuza vinyango na ni biashara hii ambayo imekuwa ikimpatia riziki yake ya kila siku.

“Mimi ninauza bangili, champali za kiasili, vinyago na vikombe vilivyodonwa kwa urembo wa kiasili na kitamaduni. Ni biashara ambayo sasa imekuwa sehemu ya maisha yangu na ninarauka hapa kila asubuhi kujikimu,” akasema Bw Shiundu.

Alisema kuwa wengi wa wateja wake ni watalii ingawa pia wenyeji wamekuwa wakinunua bidhaa kutoka kwake.

“Mimi hupata malighafi ya kuunda sanamu kutoka katika kaunti ya Kisii. Huko ndiko kwenye mawe ambayo tunatumia kuundia bidhaa hizi,” akasema.

Hata hivyo, kwa bangili na mikufu, jamaa huyu alitueleza kwamba humalizia kuzifanya mwenyewe baada ya kuzinunua kutoka Nairobi.

“Hii mikufu na bangili unazoona ninanunua Nairobi na kuja kuzimalizia hapa kwa ule mfano unaotakikana,” akasema Bw Shiundu.

Hata hivyo, jamaa huyo alisema kuwa bei ya bidhaa zake hailengi aina yoyote ya mteja bali huuza bidhaa zake kuanzia Sh100 hadi Sh5,000 mara nyingi kutegemea na ukubwa wa bidhaa ambayo mteja anataka.

“Ninapouzia wenyeji, bei kidogo huwa chini ikilinganishwa na bei ambayo nitauzia watalii,” akasema.

Alisema kwa kuwa biashara yao ya kuuza vinyago huwa ya msimu, huimarika sana kati ya mwezi wa Juni-Septemba wakati watalii wanapokuwa wengi na kufurika kununua bidhaa zao.

Alisema kuwa kwa msimu huu, biashara imerudi chini kiasi kwa sababu ya ukosefu wa watalii.

“Wakati watalii wanapokuwa wengi mimi hupata kati ya Sh10,000 au Sh20, 000 kwa siku nikiuza vyema. Lakini kwa wakati huu kidogo biashara imerudi chini. Ninashukuru kwamba hata hivyo biashara hii imenisaidia kimaisha,” akasema Bw Shiundu.

Katika kibanda jirani, tulikutana na Bi Susan Kamau, mama wa watoto wawili ambaye pia amekuwa kwa biashara hiyo ya kuuza vinyago tangu mwaka wa 2006.

Aliambia ukumbi huu kwamba kupitia kwa biashara hiyo, ameweza kufundisha watoto wake wawili na anaamini kwamba ni njia mojawapo ya kujikimu kimaisha.

“Niko na wasichana wawili na wote nimewafundisha kutokana na biashara hii. Mmoja alimaliza kidato cha nne na kwa sasa ameenda kuingia katika chuo. Mwingine yuko darasa la nane na wote walikuwa wakisomea katika shule za mabweni,” akasema.

Katika kibanda chake, Bi Kamau anauza mikufu, pete, vinyago na miko ya kupikia iliyoundwa na kupambwa kwa nakshi za kiasili.

Asema kuwa katika msimu huu, biashara imekuwa chini na sio kama vile alivyokuwa akitarajia.

“Huu ni msimu wa watalii wengi na mara nyingi huja hapa kununua bidhaa. Hatujui ni kwa nini hawajafika eneo hili kwa sasa,” akasema Bi Kamau.

Na kwa Bw Stephen Kimonye ambaye amekuwa katika biashara hii kwa miaka 11 sasa, biashara hii ndiyo ambayo imemuwezesha kukabiliana na maisha na hajutii kwa muda huo wote.

Stephen Kimonye huuza vinyago kwa watalii katika barabara ya Kenyatta, katikati mwa mji wa Nakuru. Picha/ Samuel Baya

Alisema kuwa kama haingekuwa biashara hiyo ya kuuza vinyago, basi maisha kwake yangelikuwa magumu sana, ikifahamika kwamba kazi za kuajiriwa zimekuwa chini sana,” akasema.

Kama wafanyabiashara wengine wengi, yeye huuza mikifu, sanamu zilizochongwa maridadi za wanyama, miko ya kupikia ya kale na vito vingine vingi vya kiasili.

Aidha alisema kuwa bidhaa zake zimepangwa kuanzia sanamu na vinyago vidogo vidogo hadi vikubwa, vyote vikiwa na bei tofauti tofauti na pia zaidi kuhusiana na kile ambacho mteja anataka.

“Wakati wa msimu mzuri wa biashara mimi hupata kati ya Sh5,000 na Sh6,000 wakati kunapokuwa na biashara ndogo mimi hupata angalau Sh1,000,” akasema Bw Kimonye.

Biashara yawalisha wengi

Kulingana na katibu wa muungano wa wauzaji bidhaa hizo Bw Thomas Osoro, biashara hii imewalisha wengi na ni mojawapo ya biashara tegemezi kwa asimilia kubwa ya wakazi.

Bw Osoro amekuwa katika shughuli hizi za kuuza vinyago hivi na vikapu maarufu vya kiondo kwa takribani miaka 20, na alisema biashara hii ndiyo pekee anayotegemea kuilisha familia yake.

Kwa muda huo wote, alisema amekuwa akifanya biashara zake katika maeneo ya Kampala, Mombasa, Kilifi, Malindi, Arusha na hata Dar-Es-Salaam.

“Miaka ya nyuma, biashara hii ilikuwa mojawapo ya biashara maarufu sana lakini tangu masuala ya ugaidi yalipoanza kuchacha miaka ya tisini, watalii walianza kususia kuja Kenya na hapo ndipo biashara hii ilianza kuyumba,” akasema Bw Osoro.

Alisema njia ya pekee ni kwa serikali ya kaunti ya Nakuru kuanza mikakati ya kutangaza biashara zao ili kuhakikisha kwamba wanaendelea kupata wateja.

Naye afisa mkuu wa biashara na utalii katika kaunti ya Nakuru Bw Hussein Adan alisema kuwa kaunti iko tayari kuwasaidia wauzaji hao wa vinyago.

Hata hivyo alisema bado wanasubiri mswada ambao uko bunge kwa lengo la kuangalia njia mwafaka zaidi ya kuwasaidia.