Biashara sasa zabuni mbinu kuepuka hasara

Biashara sasa zabuni mbinu kuepuka hasara

BARNABAS BII na CHARLES WASONGA

WAFANYABIASHARA nchini wamebuni mbinu mbalimbali kuhakikisha kuwa hawapati hasara kubwa kufuatia kupanda kwa bei ya mafuta, bidhaa za kimsingi na gharama ya maisha kwa ujumla.

Kwa mfano, wenye vibanda vya kuuza vyakula mjini Eldoret, wamesitisha kwa muda, utoaji wa nyongeza ya ugali kwa wateja wao, almaarufu “ugali saucer’ ili kupunguza hasara.

Nao baadhi ya wahudumu wa matatu jijini Nairobi, wameanza kubeba abiria kupita kiasi baada ya bei ya mafuta kuongezwa kwa Sh9 kwa lita, ili kupunguza hasara.

Wenye biashara ya vyakula Eldoret, wanasema wamesimamisha utoaji “ugali saucer” baada ya kupanda kwa bei ya unga hadi kuzidi Sh200 kwa pakiti moja ya kilo mbili kufuatia uhaba wa mahindi nchini.

Hali hiyo imechangia kupanda kwa bei ya mahindi, ilhali msimu wa mavuno uko mbali.

“Tafadhali zingatia kuwa ‘ugali saucer’ imesimamishwa hadi wakati usiojulikana kutokana na uhaba wa mahindi ambao umeathiri vibaya biashara yetu,” ikasema notisi katika kibanda kimoja cha kuuza chakula mjini Eldoret.

Wakati huu, bei ya mahindi imepanda hadi kufikia Sh5,200 kutoka Sh4,600 kwa gunia la kilo 90, mwezi Mei.

“Hatuna njia nyingine ila kusimamisha utoaji wa ‘ugali saucer’ kwa wateja wetu kufuatia kupanda zaidi kwa bei ya unga. Hii ndio njia ya pekee itakayotuwezesha kudumu katika biashara,” akasema Susan Too, ambaye ni mmiliki wa mkahawa mjini Kapsabet Kaunti ya Nandi.

Wamiliki wa kampuni za kusaga unga wameonya kuwa bei ya unga itaendelea kupanda katika siku zijazo kutokana na uhaba wa mahindi hata katika mataifa jirani ya Uganda na Tanzania.

“Wananchi wanafaa kuwa tayari kugharimika zaidi kupata unga kwa sababu imekuwa vigumu kwetu kupata mahindi kwa bei nafuu,” akasema Bw Kipngetich Mutai mkurugenzi wa kiwanda cha kusaga unga cha Ineet mjini Eldoret.

Nao wauzaji vyakula katika mitaa mbalimbali jijini Nairobi, pia wamepunguza ukubwa wa chapati na mandazi ili wadumishe wateja wao na kuendelea kupata faida.

“Imetulazimu kupunguza ukubwa wa mandazi na chapati bila kupandisha bei ili wateja wetu wasitoroke ili tuendelee kudumu katika biashara,” Bw Cosama Mutiso, mmiliki wa kibanda cha kuuza vyakula katika mtaa wa Mukuru Kayaba, alieleza.

Kwa upande wao, wahudumu wa matatu katikati mwa jiji la Nairobi na mitaa mbalimbali, wameanza kubeba abiria kupita kiasi nyakati za usiku ili kufidia gharama ya kupanda kwa mafuta.

“Ingawa wakubwa wetu juzi walitangaza kuwa tunafaa kuongeza nauli kwa kati ya Sh20 na Sh50, itakuwa vigumu kutekeleza nyongeza hiyo. Hii ndio maana tumeamua kubeba abiria wa kusimama saa za usiku kupunguza hasara,” akasema kondakta mmoja wa matatu ya kuelekea mtaa wa Dandora.

Kulingana na bei mpya iliyotangazwa na Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta (EPRA) Juni 14, lita ya petroli itauzwa kwa Sh159.12 kwa lita, dizeli ikiuzwa kwa Sh140 huku ya mafuta taa ikiuzwa kwa Sh127.94 jijini Nairobi.

Kuanzia Mei 14, petroli ilikuwa ikiuzwa lita moja kwa Sh150, dizeli Sh134.6 huku ya mafuta taa yakiuzwa kwa Sh120 Nairobi na maeneo ya karibu.

  • Tags

You can share this post!

Mwendeshaji baiskeli Kariuki atawala Migration Gravel Race...

Mwilu aonya wanaoendeleza ndoa za mapema Narok

T L