Makala

BIASHARA: Si haki serikali kuzuilia bidhaa za wafanyabiashara wadogo bandarini -Wabunge

October 18th, 2018 3 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE kutoka eneo la Mlima Kenya Jumatano waliitaka serikali kuingilia kati ili bidhaa za wafanyabiashara wa humu nchini za thamani ya Sh12 bilioni zilizozuiliwa katika Bandari ya Mombasa ziachiliwe.

Wakiongea na wanahabari katika majengo ya bunge Jumatano, wabunge hao waliitaka Serikali Kuu kuamuru kuachiliwa kwa bidhaa hizo zilizoagizwa kutoka nje na wafanyabiashara wadogo wadogo.

Bidhaa hizo zimekuwa zimeagizwa na wafanyabiashara hao kutoka mataifa ya ng’ambo na zimekwua zikizuiliwa katika bandari ya Mombasa kwa miezi miwili kwa madai kuwa baadhi yazo ni ghushi.

Wabunge walioibua malalamishi hayo ni pamoja na; Ndindi Nyoro (Kiharu), Gathoni Wa Muchomba (Mbunge Mwakilishi wa Kiambu), James Gakuya (Embakasi Kaskazini), Benjamin Mwangi (Embakazi ya Kati), Jude Njomo (Kiambu), Anthony Kiai (Mukweini), Catherine Waruguru (Mbunge Mwakilishi wa Laikipia) na George Kariuki (Ndia).

Walilaumu mashirika ya serikali kama vile Mamlaka ya Ukusanyaji wa Ushuru Nchini (KRA) na Shirika la Kupambana na Bidhaa Feki (Kebs) kwa kuwapendelea wafanyabiashara matajiri na kupuuzilia mbali masilahi ya wafanyabiashara wadogo.

“Tunataka KRA na Kebs kutueleza kama hii sheria kuhusu bidhaa feki inatumika kwa wafanyabiashara wadogo pekee huku wake wakubwa wakisazwa? Mbona wanawatesa wafanyabiashara wadogo kwa kusingizio cha kupambana na bidhaa ghushi kutoka ng’ambo? ” akauliza Bw Nyoro.

Alisema licha ya makubaliano mbalimbali kati ya wafanyabiashara hao na serikali na wafanyabiashara hao, bidhaa za wafanyabiashara hao zimekuwa zikiendelea kuzuiliwa bandarini tangu mwezi Julai mwaka huu.

“Mwezi jana wafanyabiashara hawa waliokutana na maafisa wa KRA na Kebs mbele ya Mkuu wa Watumishi katika Afisi ya Rais Bw Nzioka Waita na wakakubaliana kumaliza mzozo huu. Lakini miezi miwili mpaka sasa bidhaa za wafanyiashara hao hazijaachiliwe. Hii sio haki kwani wengi wanaendelea kupata hasara huku mashiriki ya kifedha yaliyowapa mikopo yakiendelea kudai pesa zao,” akasema Bw Njomo.

“Wafanyabiashara wadogo ambao huagiza bidhaa kutoka ng’ambo wameumizwa zaidi ya amri ya hivi punde ya KRA kwamba bidhaa feki zikipatikana ndani ya konteina miongoni mwa zile halali, kontaina nzima itaharibiwa. Amri hii ni dhalimu na inapasa kuondolewa mbali,” akasema.

Mnamo mwezi Juni Rais Kenyatta aliingia kati mzozo huo na kuamuru kwamba wafanyabiashara hao wasitozwe ada ya gharama ya uhifadhi wa bidhaa zao zilizozuiliwa na asasi hizo ambazo zimekuwa zikiendeleza operesheni dhidi ya bidhaa ghushi.

Aliwaamuru maafisa wa asasi hizo kuharakisha ukaguzi wa bidhaa hizo ili zile ambazo ni halisi wenye waruhusiwe kuzichukua.

“Hatutaki wafanyabiashara wetu kuendelea kuathirika huku maafisa wa KRA na KEBs wakiendelea kujikokota katika kazi ya kukagua bidhaa zilizozuiliw bandarini,” Rais Kenyatta akasema siku mbili baada ya wafanyabiashara hao kufanya maandamano jijini Nairobi kulaani kuzuiliwa kwa bidhaa hizo.

Mbunge Mwakilishi wa Laikipia Catherine Waruguru (kushoto) akiwa na Gathoni Wa Muchomba, Mbunge Mwakilishi wa Kiambu walipohutubia wanahabari Oktoba 17, 2018. Picha/ Charles Wasonga

Wakati huo huo, wabunge hao, kutoka kaunti za Nairobi na wamezitaka serikali za kaunti zisitoa leseni za kibiashara reja reja kwa wageni wakisema biashara hizo zinapasa kuachiwa Wakenya.

Haswa walikerwa na mwendo wa Wachina kuingilia biashara za reja reja ambazo walisema zinafaa kuendeshwa na Wakenya, haswa vijana ambao wengine wao hawana ajira licha ya kuhitimu kwa shahada mbalimbali.

Vile vile, waliitaka Serikali ya Kitaifa kufutilia mbali vyeti vya kazi kwa wageni ambao hufanyakazi ambazo Wakenya wamehitimu kufanya.

“Asilimia 55 ya vijana nchini hawana ajira. Hii ndio wengi wao wameingilia biashara ndogo ndogo za uchuuzi. Hatatuka watu kutoka China kuja hapa nchini na kushindana na watu wetu katika biashara ya kuuza bidhaa ambazo zimetengenezwa kwao na kuingizwa humu nchini,” akasema Bi Waruguru.

“Kwa hivyo, tunazitaka serikali zote za kaunti, zikiongozwa na Serikali ya kaunti ya Nairobi kufutilia mbali leseni za kibishara kwa Wachina hao ambao wamezagaa katika miji kadhaa nchini wakishindana na Wakenya,” akaongeza.

Naye Bw Njomo alimtaka mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu Biashara Bw Kanini Kega kufuatilia suala hilo na maafisa husika katika serikali kuu na zile za kaunti ili kuhakikisha kuwa masihali ya wafanyabishara wa asilii ya Kenya yanalindwa.

“Ikiwa hakuna Mkenya ambaye huruhusiwa kufanya biashara nchini China, mbona Wachina wapewe nafasi hiyo humu nchini huku watu wetu wakiseka. Tunataka Bw Kega na kamati yake kuhakikisha kuwa biashara zote za reja reja zinaendesha na Wakenya wala sio wageni,” akasema.