Michezo

Biashara United kutema wachezaji 10

June 6th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Francis Baraza wa Biashara United mjini Mara, Tanzania, amesema atalazimika kuwatema kikosini wachezaji 10 na kujinasia maarifa ya wengine watano katika juhudi za kuisuka upya timu yake kwa minajili ya Ligi Kuu msimu ujao.

Hadi kusimamishwa kwa soka ya Tanzania mnamo Machi 2020 kwa sababu ya janga la corona, Biashara United walikuwa wakining’inia pembamba mkiani mwa jedwali baada ya kusajili ushindi mara mbili, kupiga sare mbili na kupoteza mechi sita kati ya 10 walizokuwa wamesakata.

Kwa mujibu wa Baraza ambaye amewahi kuchezea timu ya taifa ya Harambee Stars, kikosi cha Biashara Utd kina idadi kubwa zaidi ya wachezaji, jambo ambalo linamtatiza katika utekelezaji wa majukumu yake ya kuinoa timu itakikanavyo.

“Timu ina wanasoka wengi. Ili ianze kufanya vyema, italazimu usimamizi kupunguza zaidi wachezaji kutoka 31 waliopo. Nahitaji kikosi cha angalau wachezaji 26 au 27 pekee kwa minajili ya msimu ujao. Hili litatuweka katika ulazima wa kuagana na masogora 10 na kusajili wengine watano katika muhula ujao wa uhamisho,” akasema Baraza.

Tangu apokezwe mikoba ya Biashara Utd mnamo Novemba 2019, Baraza amewaongoza waajiri wake kusajili ushindi katika mechi tisa na kupoteza tatu pekee kati ya 19 zilizopita.

Kabla ya Ligi Kuu ya Tanzania kusitishwa kwa muda usiojulikana kutokana na janga la corona, Biashara Utd walikuwa katika nafasi ya 10 baada ya kujizolea jumla ya alama 40. Ligi hiyo imepangwa kuanza upya mnamo Juni 13 baada ya Serikali kulegeza baadhi ya masharti ya kudhibiti ya maambukizi ya virusi vya corona.

“Naridhishwa na kiwango cha kujituma kwa wachezaji, nidhamu yao na ushindani ambao wamekuwa wakidhihirisha hata katika vipindi vya mazoezi,” akasema Baraza kwa kusisitiza kwamba kubwa zaidi katika maazimio yao ni kukisuka upya kikosi chake na kuimarisha uthabiti wa kila idara.

Kati ya mechi 29 ambazo zimesakatwa na Biashara Utd katika mashindano yote ya msimu huu, kikosi hicho kinacholenga kukamilisha kampeni za msimu huu ndani ya mduara wa nane-bora jedwalini, kimesajili ushindi mara 10, kuambulia sare mara 10 na kupoteza jumla ya mechi tisa.

Baraza alijiunga na Biashara Utd msimu huu kutoka Chemelil Sugar ambao kwa pamoja na Kisumu All-Stars na SoNy Sugar, wameshushwa ngazi kutoka Ligi Kuu ya Kenya (KPL) hadi Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL) muhula ujao.