Makala

'Biashara ya mutura na supu ina faida'

July 12th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

BIASHARA ya kuuza mutura na supu imepata umaarufu mkubwa katika mitaa mingi nchini Kenya.

Katika mtaa wa Kambi ulioko katika Kaunti ndogo ya Kigumo ndani ya Kaunti ya Murang’a, tunakutana na Bw Julius Nyutu ambaye kwa miaka ielekeayo 20 amekuwa katika biashara hii na amejijengea ploti yake ya thamani ya Sh3 milioni katika soko la sasa.

Anasema kuwa ni biashara ambayo huhitaji mtaji wa chini kwa kwani “ukiwa na Sh5,000 tayari uko pazuri kuianza.”

Anasema ni kuanzia mwaka wa 2000 ndipo matumbo ya mifugo katika vichinjio yalianza kuuzwa.

“Awali tulikuwa tukiyachukua tu kama nyama zisizo na maana na kuzigeuza kuwa pato kwetu,” anasema Bw Nyutu.

Anasema kuwa malighafi ya uundaji mutura hulingana na mapenzi yako kama mwandalizi.

“Kuna baadhi wataweka viazi ndani ya hayo matumbo, wengine waweke nyama huku wengine wakiamua kuweka vitunguu na hata damu,” anasema.

Katika hali zote, anasema utamu wa biashara hii ni kuwa mfanyabiashara atahitaji tu jiko, sufuria, maji na chumvi na kisha ajitokeze mahali palipo na wateja na aanze kutumia lugha ya kuwavutia wateja.

“Harufu tu ya mutura ukikauka juu ya moto na supu ikichemka ni tangazo tosha la kibiashara. Kazi yako tu ni kupima mutura wa Sh10 kwenda juu na ukipata aliye na Sh5 pia, karabati kipimo bora tu usiachilie pesa zikupite,” anasema.

Anasema kuwa malighafi hayo hupatikana katika vichinjio hapa nchini na wakati wafugaji wamechinja nyumbani kwao, unaenda kununua hayo matumbo na nyama zingine ambazo hazihitajiki sana katika lishe ya walio na ubaguzi wa mlo wa nyama.

“Ngozi, miguu na kichwa ni miongoni mwa nyama ambazo wengi hutupa… Lakini ukizipata, wewe uko katika njia ya kuunda faida kwa haraka,” anasema.

Ajijenga

Katika hali hiyo, Bw Nyutu ambaye pia ni kasisi katika dhehebu la dini ya Akorino anasema kwa siku huunda takriban Sh2,000 kutoka kwa biashara hii na ambapo kwa kuwa haendi mtaani kufuja pesa zake kwa ulevi na mengine ya raha, anajipata akijijenga.

“Nimeelimisha watoto wangu na biashara hii ya mutura na supu na pia kujifadhili katika miradi yangu ya kujiimarisha. Nikiwa na umri wa miaka 60 kwa sasa, nalenga kuwa katika biashara hii hadi Mungu anijalie uzee wa kukosa nguvu za kustahimili joto la upishi…” anasema.

Anaongeza kuwa kwa sasa biashara hii hupata kivutio kikuu ikizingatiwa kuwa ukihitaji kula nyama, itakubidi uwe na pesa zisizopungua Sh50 lakini ukiwa na Sh10 hukosi ladha ya mutura.

Anaongeza kuwa kazi ngumu mashinani huwapa wanaozifanya shinikizo za kujenga miili yao na ambapo supu ni mojawapo ya lishe ambayo imejishindia katika safu hiyo.

Pia, anasema kuwa udogo wa uchumi mashinani na pia katika mitaa ya mabanda huifanya biashara hii kuwa maarufu “kwa kuwa kunao watanunua supu ya Sh20 na iwe ndiyo mboga ya familia ya watu 10 kula sima.”

Bw Nyutu anasema kuwa licha ya wengi kusambaza habari za uongo kuhusu hii biashara ya supu na mutura, “imebakia ngangari ikijinyanyua kutoka kwa kila aina ya propaganda za kuimaliza.”

Anasema kuwa kuna baadhi husema kuwa baadhi ya wauzaji supu na mutura husaka nyama kiharamu hata kutoka kwa mizoga barabarani.

“Wengine husema kuwa vitengo vya afya ya umma vinafaa kutumulika kwa ukali ili tupunguziwe umaarufu. Lakini hao wanaosambaza mito hiyo hawasemi maafisa hao wasukume watupao chakula katika mapipa wawajibikie hali kwamba chokoraa hujipa lishe kutoka kwa mapipa hayo,” anasema.

Anasema: “Mungu ndiye hutukinga kutokana na athari za hatari katika lishe kwa kuwa hata wale ambao hula mapochopocho ya kifahari huugua saratani.”

Katika hali hiyo, anasisitiza biashara ni biashara bora iwe halali na ambayo inazingatia maadili ya kimsingi ya kumfahamisha anayeiendesha kuwa analisha binadamu wala sio wanyama.