Habari

Biashara ya nyama yanoga kisiwani Lamu

May 8th, 2020 1 min read

Na KALUME KAZUNGU

BIASHARA ya nyama katika mji wa kale wa Lamu imekuwa ikifanya vyema tangu Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ulipoanza licha ya kuwepo kwa pandashuka za janga la Covid-19.

Wamiliki wa maduka ya nyama kisiwani Lamu wamekiri Ijumaa kwamba wanauza nyama kwa wingi hasa mchana na nyakati za jioni tangu Ramadhani ilipoanza wiki moja iliyopita.

Katika mahojiano na Taifa Leo wamiliki hao hasa wa mitaa ya Langoni, Mkomani, Gadeni, Wiyoni, Kashmir na sehemu zingine, wamesema mara nyingi wateja wao, wengi wao wakiwa Waislamu, wamekuwa wakiunga foleni ili kujinunulia nyama kwa matayarisho ya futari.

Bw Ali Hassan hakuficha furaha yake kutokana na faida ambayo amekuwa akivuna kufuatia kunoga kwa biashara ya nyama mjini Lamu.

“Mimi nimekuwa nikifunga duka langu la nyama kufikia saa nane mchana kila siku. Nyama zimekuwa zikiisha haraka na tunashuruku kwa hilo kwani limetufanya kurekodi faida chungu nzima,” akasema Bw Hassan.

Naye Bw Mohamed Alwy ambaye ni mmoja wa wauzaji wa nyama kisiwani Lamu amesema anafikiria kuongeza kiasi cha nyama ambayo amekuwa akiuzia wateja wake hasa kufikia juma lijalo kwani wateja wameongezeka maradufu.

“Juma hili wateja wamekuwa wakifurika kwa wingi kibandani mwangu kununua nyama hasa majira ya jioni. Wengibne ewamekuwa wakikosa nyama kwani shehena ilikuwa kidogo. Nimefikiria kuongeza shehena kufikia juma lijalo,” akasema Bw Alwy.

Kilo moja ya nyama huuzwa kwa hadi Sh600 kisiwani Lamu.