Makala

BIASHARA YA UREMBO: Vipepeo wanavyovutia watalii Pwani

August 25th, 2019 4 min read

NA RICHARD MAOSI

Mombasa Butterflies House katika eneo la Fort Jesus, Mombasa, ni maarufu barani Afrika kwa utunzaji wa spishi mbalimbali za vipepeo wanaotumika kuvutia watalii na kuwapa wenyeji kipato.

Ni mradi wa ubunifu kwa wakulima wadogo kutoka mashinani wasiokuwa na uwezo mkubwa kiuchumi kujiendeleza kimaisha mbali na kuhifadhi misitu ya asilia.

Ni bayana ukataji miti kiholela umesababisha aina fulani ya vipepeo kuwa nadra duniani, na ipo haja ya mbinu mbadala za kuhakikisha kuwa hawaangamii.

Mombasa Butterflies House inayosimamiwa na Idara ya Makavazi nchini, ilianzishwa mnamo 2014, kwa madhumuni ya kuhifadhi msitu wa Arabuko Sekoke unaopatikana katika Kaunti ya Kilifi.

Aidha, waasisi walipania kuwahimiza wakulima watumie malighafi ya misitu kwa busara, ili Arabuko Sekoke iwe ya manufaa kwa vizazi vya baadaye.

Bi Momo Faki, mhudumu katika jumba la Mombasa Butterflies House akionyesha spishi mbalimbali za vipepeo wanaonunuliwa kwa wakulima na kuzaana. Picha/ Richard Maosi

Idara hiyo ilitumia hekima za wakazi wa Kilifi, wengi wao wakiwa ni wale wanaotegemea bidhaa za misitu kama vile kuni, asali na dawa za kiasili kukidhi mahitaji.

Katika mpango huo wakazi wa Kilifi walisaidia wanasayansi na watafiti kutambua miti maalum inayositiri aina mbalimbali za mayai ya vipepeo.

“Kwa desturi wakiendea mti fulani wakazi wanafahamu kuna aina fulani ya vipepeo,” Bi Momo Mfaki mhudumu wa Butterflies House Mombasa aliambia Taifa Leo Dijitali.

Alieleza kuwa soko la kimataifa hasa Uchina, limekuwa likiagiza watoto wa vipepeo kwa bei nzuri inayowapa wakulima tija, na masalio kuchukuliwa na makavazi ya Butterflies House.

Bi Faki anasema vipepeo wanapenda kula malimau na wakati mwingi machungwa miongoni mwa lishe nyinginezo kama vile majani. Picha/ Richard Maosi

Bi Momo alieleza kuwa mataifa ya nje yanapendelea spishi mbalimbali za vipepeo za humu nchini, kwa sababu huwa maridadi na wakati mwingine vipepeo kutoka Kenya wanatumika kufanyia utafiti.

Kulingana naye, hii ni njia mojawapo ya kuhifadhi misitu wanamokulia vipepeo. Alieleza kuwa kazi ya makavazi ni kununua mayai ya vipepeo na kuyahifadhi ili yazaane ndani ya Butterflies House.

Vipepeo wanapokomaa hutumika kama kivutio kwa watalii na wageni wanaolipa ada fulani kujivinjari ndani ya jengo hili lililostawishwa na juhudi za wakulima wa vipepeo.

Momo alieleza kuwa yai huchukua baina ya siku 3-5 kuangua, baadaye huchukua wiki mbili hivi kwa kipepeo mdogo kukomaa hadi akue kipepeo mzima.

Wakulima pia hufundishwa mambo mengine mengi kuhusu uhifadhi wa mazingira. Picha/ Richard Maosi

“Wakati kipepeo akiwa mdogo anapenda kula chembechembe zinazotokana na machungwa na malimau na akishakomaa huanza kutafuna majani mepesi,” alisema.

Baadhi ya wakulima huvuna na kusafirisha vipepeo wadogo na kuwapeleka kwenye masoko yanayopatikana Pwani kama vile Gede Kipepeo Local Market.

Kipepeo mmoja huuzwa kwa Sh50 sokoni humo, lakini wakiuzwa kwa bei ya rejareja ni Sh30. Wakulima wengi kutoka milimani hasa Taita Taveta na Kwale wameamua kujihusisha na kilimo hiki cha kufuvuna vipepeo ambacho ni sanaa nadra inayohitaji ujuzi wa aina yake.

Bi Momo anasema kwenye soko la kimataifa wakulima huuza bidhaa zao kwa Dola za kimarekani, na bila shaka wao huchuma hela ndefu kuliko soko la humu nchini ambalo linaendelea kukua.

Baadhi ya bidhaa nyinginezo ambazo wao hununua kutoka kwa wakulima ni pamoja na asali ya msituni,sabuni na awa za kiasili. Picha/Richard Maosi

“Kwenye makavazi ya Butterfly House Mombasa kipepeo mtoto hununuliwa kwa Sh70, hivyo basi kila mkulima anaweza kuvuna hadi Sh100,000 kwa mwezi kulingana na bidii yake,” akasema.

Ni kwa sababu hiyo wakulima wengi kutoka Kilifi wamepania kuungana kama makundi na kuvuna watoto wa vipepeo kwa pamoja kisha kuuzia makavazi kutoka pwani, ambayo pia huwasaidia kuwatafutia masoko ulaya.

Momo anasema ingawa kazi yenyewe inahitaji moyo, watu wengi wameendelea kuchapukia swala hili kama njia mojawapo ya kujiajiri na kuwaajiri wengine.

Bi Edith Mwangeka, mkazi wa Kilifi na mfanyibiashara wa vipepeo, anasema wakulima wakiendelea na shughuli kama hizo misitu yote nchini italindwa dhidi ya uharibifu.

Anaona ndio njia ya kipekee ambapo wakulima wataendelea kuzumbua riziki kutokana na misitu bila kuharibu malighafi haya ambayo husaidia kuvuta mvua na kusafisha hewa.

Akiwa mama ya watoto watatu anasema kilimo cha vipepeo kimemsaidia kushirikiana na mumewe kusomesha watoto,kununua ploti na kuanzisha miradi mingine yenye manufaa kama ufugaji kuku.

“Sisi kama wakulima tumefaidika na mafunzo kutoka kwenye mashirika ya kuhifadhi misitu kwa ushirikiano na makavazi ya humu nchini,” alisema.

Akiwa mwenyekiti wa kikundi cha akina mama 14 anasema kwa mwezi mmoja wanaweza kutengeneza hadi Sh300,000, na hela hizi zimekuwa zikitumika kuwaongezea mtaji.

Bi Mwangeka anawashauri wakulima wanaolenga kuzamia katika aina hii ya kilimo,kukuza aina mbalimbali ya miti kwenye maboma yao ili watoto vipepeo wapate chaguo la lishe za kutosha.

Hii ni sehemu inayotiririka maji ambapo vipepeo hutumia wakati wao mwingi wakati wa mapumziko. Picha/ Richard Maosi

“Wakati mwingi vipepeo huona afadhali kula machungwa na malimau ikiaminika kuwa ni lishe inayowafanya wao kukomaa haraka na kuongeza kilo kabla ya kusafirishwa sokoni,” alisema..

Mwangeka alitufichulia kuwa amekuwa akipata ujuzi wa kubaini aina ya vipepeo endapo ni wa kike au kiume kwa sababu wale wa kike wanapenda kuruka kutoka kwenye mti mmoja hadi mwingine wakitafuta sehemu ya kutaga mayai.

Changamoto

Kila biashara huja na faida ama hasara, na hili limebainika kuwa kweli katika ulingo wa biashara ya vipepeo.

Kulingana na Bi Momo Mfaki,anasema wakati wa kusafirisha vitoto vipepeo sokoni, kipepeo mmoja anaweza akakomaa mbele ya wenzake kisha akasababisha hasara kwa kuwala wale wengine wadogo.

Butterfly House. Picha/ Richard Maosi

Ndio maana wakulima watahitaji kupatiwa ujuzi wa kutosha kuhusu muda unaohitajika kukuza vipepeo ili waje kukomaa kwa muda mmoja.

Pili baadhi ya vipepeo huletwa katika makavazi ya Butterfly House wakiwa wana maradhi ambayo yanaweza kusambaa na kuangamiza vipepeo wengine wanaoendelea kukua.

Hii huwa ni hasara kwa mnunuzi na faida kwa mkulima kwani pindi wanapohesabiwa, mnunuzi hawezi kurejesha viumbe hawa kwa muuzaji wakiwa na maradhi.

Tatu wanyama kama vile mjusi, nyoka na panya hulenga kula mayai ya vipepeo ambayo ni laini na yenye ladha nzuri. Endapo hayatahifadhiwa vyema basi huenda mnunuzi akakadiria hasara .

Aidha kitu ghali zaidi ni kununua vipepeo, kwani hii ni biashara inayoendelea kupata mashiko humu nchini hasa maeneo ya pwani, jambo linalofanya bei yake kupanda kwa kasi.

Pia anasema endapo aina fulani ya vipepeo imejaa sokoni, mauzo huteremka jambo linaloweza kuwafanya wakulima kuuza bidhaa yenyewe kwa bei ya kutupa na kupata hasara.

Hata hivyo anawashauri vijana wengi kutoka pwani kujitosa katika ulingo huu wa kipekee ili kujitafutia njia mbadala ya kujikimu kimaisha badala ya kutegemea nafasi chache za ajira zinazopatikana.