Makala

BIASHARA YA USANII: Burudani ilivyowavumbulia ajira

June 27th, 2019 3 min read

Na RICHARD MAOSI

KATIKA kukabiliana na changamoto za maisha, zipo mbinu nyingi ‘halali’ za kujipatia kipato kama vile ujuzi wa kucheza ala za muziki kwa malipo.

Huu ndio wosia wa mtumbuizaji nguli kutoka mjini Nakuru, George Ogolla Oula mwasisi wa kundi la Agora,linalotumia burudani ya kucheza ala za muziki kama kazi .

Ogolla anasema aliasisi mradi wenyewe 2015 kuinua vijana wenye vipaji kutoka mitaani, ili wajiajiri na kuwa watu wa maana katika jamii.

Anaamini kuwa chochote unachokifanya kwa bidii, ni lazima utakuja kufanikiwa muradi tu uwekeze, ukifahamu tijara yoyote ina faida na wakati mwingine hasara.

Uwezo na umahiri alio nao kijana huyu katika uimbaji na upigaji wa ala za muziki kama kazi umemfanya kukutana na watu wenye haiba kubwa katika daraja mbalimbali za maisha akiwemo rais.

Upigaji ala za muziki umemsaidia kufanya uwekezaji, kuanzisha lebo yake ya muziki na kumiliki biashara ya vipodozi kwenye juhudi za kujiimarisha kimaisha.

Alianza kujihusisha na upigaji vyombo akiwa kijana mdogo, lakini alipofika umri wa miaka 12, akajifundisha kupiga gitaa.

Baada ya kuonyesha ushupavu alitambuliwa na serilkali ya kaunti ya Uasin Gishu mnamo 2015, na ile ya Nakuru kwa kuchangia katika hazina ya vipaji na ajira miongoni mwa vijana.

Mafunzo anayotoa kwa vijana ni kupiga ala za muziki zikiwemo, gitaa, tarumbeta, zeze, kayamba, marimba, ngoma za kiasili, piano na kutathmini ubora wa sauti.

Mafunzo yake hufanyika katika maeneo yaliyo wazi kama vile bustani za umma, makanisa au kumbi za tamasha. Hili limemsaidia kukata gharama kubwa ya kukodi vyumba vya kuendeshea operesheni zake.

“Mimi na wenzangu pia tunajifundisha kucheza densi kupitia miondoko ya kitambo na ya kisasa ili kufikia hadhira pana zaidi,” anasema.

Anawahimiza vijana kuwa mbali na kutumia wakati wao mwingi kutazama filamu, kwa nini wasishiriki kwenye tamasha za kujifundisha namna ya kucheza ala za muziki?

Kupitia midundo anayobuni, anawahimiza vijana kubadili mienendo yao na kufanya uteuzi unaofaa.

Kufikia sasa katika chuo chake cha muziki (Agora) amefikisha wanafunzi 42 ambao wamegawika kwenye makundi matatu.

Wapo waliokubuhu katika upigaji wa ala za muziki, waimbaji na wale wanaotunga kazi za kuwakilishwa kwa ajili ya hafla tofauti.

Anasema kuwa kitu chochote kinachoweza kutoa sauti kinaweza kutumika kama ala za muziki, hata sauti ya binadamu inatajwa kama ala ya muziki.

Mwanzoni haikuwa rahisi kujitosa katika ulingo wenyewe akisema alikumbana na changamoto nyingi kabla ya kukubalika.

Anasema kukataliwa ni pandashika zinazoweza kumpata mjasiriamali yeyote.

Alifanikiwa kushawishi vijana watatu kutoka Naivasha, Freearea na London mjini Nakuru walioamua kujiunga naye ili kuanzisha bendi.

Shughuli zao nyingi ni kuzuru vyuo, harusi, mazishi, shule za msingi na upili.

Wakiwa watumbuizaji, wachoraji, malenga na waimbaji stadi, sanaa ya kupiga ala za muziki ndiyo inawatofautisha na makundi mengine ya burudani nchini Kenya.

 

George Ogolla Oula kutoka Kaunti ya Nakuru amfunza mmoja wa wanafunzi wake jinsi ya kucheza ala za muziki. Picha/ Richard Maosi

Kwanza alifanya utafiti kuhusu aina ya muziki ambao watu wengi nchini wanapenda kusikiliza, ndiposa akaunda midundo ya vibao hivyo.

Pia anasema kusikiliza muziki wa wasanii wengine, kulimsaidia kupanua mawazo na kuelewa njia mbalimbali za kutumbuiza hadhira.

Makali yao jukwaani yakionekana kufanikisha sherehe za kitaifa uwanjani Afraha, ikiwemo Siku ya Mashujaa, Madaraka, Leba Dei miongoni mwa hafla nyinginezo zenye hadhi.

Burudani kwa wageni

Viongozi wa kaunti wamekuwa wakitumia huduma za Agora kuwaburudisha wageni wanaofika Nakuru kutalii; hasa wa kutoka ukanda wa jumuia ya Afrika Mashariki.

Mbali na kujijengea jina, wamehusika katika shughuli za kutangaza bidhaa kama vile mafuta ya kujipaka, taasisi za elimu na huduma za simu kwa wateja.

Mashabiki wao ni vijana na wazee, wa kila umri na rika kutoka ndani na nje ya kaunti ya Nakuru.

“Sio watu wengi wanaweza kuamini kuwa mtu anaweza kujiajiri, kutokana na upigaji wa vyombo vya muziki,” anasema.

Kwa miaka mitatu wamekuwa wakicheza ala za muziki na kujifundisha ustadi wa kunengua viuno kwa kuzingatia mitindo ya kisasa.

“Kazi zetu nyingi humulika siasa, bidii na kazi, nafasi ya mwanamke katika jamii, umaskini, elimu na utunzaji wa mazingira,” Dominic anasema

Ni vijana waliojiendeleza kwani wao hujirekodia vibao, na kujitangaza kupitia mitandao ya kijamii, ukumbi unaowafikia vijana wengi.

Kadri siku zinavyosonga wasanii wengi wanatamani kufanya kazi naye wakiamini kuwa ni kijana mwenye maono ya mbali.