Biashara za hoteli, gesti zanoga Mokowe miaka mitatu baada ya bandari ya Lamu, barabara kukamilika

Biashara za hoteli, gesti zanoga Mokowe miaka mitatu baada ya bandari ya Lamu, barabara kukamilika

NA KALUME KAZUNGU

BIASHARA za hoteli na gesti zinazidi kuchipuka na kunoga eneo la Mokowe, Kaunti ya Lamu tangu kufunguliwa rasmi kwa shughuli za uchukuzi bandarini Lamu (Lapsset) karibu miaka mitatu iliyopita.

Kukamilika na kufunguliwa rasmi kwa barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen pia kumenawirisha biashara hiyo.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Jumapili umebaini kuwa zaidi ya hoteli na mikahawa mipya pamoja na nyumba za gesti zaidi ya 20 tayari zimekamilika na zinahudumia wateja eneo hilo, hali ambayo imeufanya mji wa Mokowe kuzidi kunawiri kibiashara.

Bandari ya Lamu, ambayo ni ya kima cha Sh310 bilioni ilifunguliwa rasmi na Rais Mstaafu, Uhuru Kenyatta mnamo Mei 20, 2021, siku ambayo pia aliifungua barabara ya kilomita 135 ya Lamu-Witu-Garsen iliyojengwa na serikali kuu kwa kima cha Sh10.8 bilioni.

Wafanyabiashara waliohojiwa na Taifa Jumapili mjini Mokowe waliishukuru serikali kwa kukamilisha miundomsingi hiyo muhimu, hasa barabara na bandari ambazo zimekuwa kivutio kwa wengi kuja Lamu.

Mkahawa mpya kwa jina Islanders Joint, Restaurant ulioko pembezoni mwa barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen eneo la Mokowe, Kaunti ya Lamu. Mkahawa huo wa kifahari ulijengwa 2021 muda mfupi baada ya kukamilika na kufunguliwa rasmi kwa bandari ya Lamu (Lapsset) na barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen. Umeibukia kupendwa na wateja wengi.
PICHA | KALUME KAZUNGU

Suleiman Abdulrahman, mmoja wa wawekezaji wa biashara ya hoteli mjini Mokowe alisema kila siku yeye hakosi wateja wasiopungua 50 kwenye mkahawa wake.

Bw Abdulrahman alisema biashara pia hunoga zaidi wakati wakuu wa serikali, ikiwemo Rais William Ruto, Naibu Wake, Rigathi Gachagua, mawaziri na wageni wengine wanapozuru Lamu kwa shughuli zao za kikazi.

“Nafurahia sana kukamilika kwa bandari ya Lamu na pia barabara yetu kuu. Miundomsingi hiyo imeboresha biashara zetu. Hoteli na mikahawa hapa Mokowe imekuwa ikifurika wateja kila siku, hasa wafanyakazi wa bandari ya Lamu,” akasema Bw Abdulrahman.

Swaleh Athman, mmiliki wa gesti moja mjini Mokowe alisema wafanyakazi wengi wa Lapsset, hasa vibarua wamekuwa wakifurika kwenye gesti yake kulala usiku, hivyo kunogesha biashara hiyo.

Bw Athman aliishukuru serikali kwa kuzidisha usalama mjini Mokowe na viungani mwake, hali ambayo imejenga imani zaidi kwa wanaozuru eneo hilo.

Eeneo la Mokowe liko na vituo kadhaa vya polisi, jeshi na maafisa wa vitengo vingine vya usalama.

“Kutokana na kwamba Mokowe imekaribia bandari yetu ya Lamu, miundomisngi mingi imeboreshwa. Isitoshe, vituo vya polisi, jeshi, majasusi na wengineo vimebuniwa hapa na hili limetuma imani kubwa kwamba eneo letu ni salama kwani limelindwa vilivyo,” akasema Bw Athman.

Fatma Bakari ambaye ni mkazi wa Mokowe alisema mbali na miundomsingi kuboreshwa, hatua ya serikali ya kuhamisha makao makuu ya serikali ya kaunti ya Lamu na ofisi za kamishna wa kaunti hiyo kutoka kisiwa cha Lamu hadi Mokowe imepandisha hadhi zaidi Mokowe kuwa eneo la kibiashara na utawala.

“Hapa Mokowe utapata ofisi ya gavana, Issa Timamy na pia makao makuu ya kamishna wa kaunti hii. Hii inamaanisha Mokowe ndiyo ikulu. Kwa sasa wengi wa wafanyakazi wa serikali kuu na ile ya kaunti huishi hapa Mokowe. Hilo ni jambo jema kwetu sisi kama wanabiashara,” akasema Bi Bakari.

  • Tags

You can share this post!

Dkt Neema Lema atumia teknolojia kutibu watoto kwa kuwapa...

Linturi aonya wakora wanaouza mbolea ya serikali

T L