Makala

Biashara zatoka soko kufuatia ada za juu za leseni

March 23rd, 2024 2 min read

NA LAWRENCE ONGARO

WAFANYABIASHARA sasa wanasema kazi yao inaharibika kutokana na sheria na sera zinazowataka kulipia ada za juu kwa leseni na vibali.

Wiki hii wafanyabiashara wapatao 100 walikutana mjini Thika ambapo walitoa wito kwa serikali ya Kaunti ya Kiambu kulainisha utaratibu wa kutoa leseni na vibali vya biashara.

Mwenyekiti wao Bw Alfred Wanyoike aliitisha kikao cha dharura ili kujadili kwa kina jinsi ambavyo biashara zimedorora pakubwa kwa mwaka mmoja uliopita tangu serikali ya Kenya Kwanza ichukue hatamu za uongozi mnamo Septemba 13, 2022.

Mkutano huo uliodumu saa tatu, ulijadili matatizo ya kibiashara na ulifanyika katika mkahawa mmoja mjini Thika mnamo Jumatano.

Kulingana nao, biashara asilimia 40 kwa wakati huu zimefungwa jambo walilosena ni hatari kwa maisha ya wafanyabiashara wengi.

Sasa wametuma ujumbe maalum kwa Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi ili wafanye kikao haraka iwezekanavyo.

Kinara huyo alisema ujumbe huo wa kufanya kikao maalum na gavana ni wa dharura.

Pia alisema Rais William Ruto anafaa kuzungumza na magavana na viongozi wengine ili mazingira ya kufanyia biashara yaimarishwe kote nchini.

Kuhusu mtindo wa baadhi ya wachuuzi wa kuuza bidhaa zao nje ya maduka makubwa ya wafanyabiashara alisema ni jambo linalokera wengi.

“Wachuuzi hao hufika mchana mbele ya maduka hayo na kuanza biashara zao hapo. Hiyo ni njia mojawapo ya kuharibia wafanyabiashara wakubwa mipango yao ya kila siku,” alilalama Bw Wanyoike.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Thika Bw Alfred Wanyoike akihutubu kwenye mkutano wao Jumatano. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Lakini pia walisema suala lingine ni kuhangaishwa na maafisa wa kaunti wakiwemo askari almaarufu kanjo.

“Tabia ya aina hiyo haikushuhudiwa katika utawala wa magavana wa hapo awali na kwa hivyo hatutakubali maafisa hao wachukue sheria mikononi mwao kwa kutunyanyasa,” alifoka mwenyekiti huyo.

Wafanyabiashara wengi hulazimika kuhepa maafisa hao ili wasisumbuliwe zaidi na maswala ya ukusanyaji wa mapato.

Walisema hata wangetaka kulindwa na maafisa wa polisi kwa sababu maafisa hao wa kaunti ya Kiambu hufika na fujo nyingi wanapoendesha shughuli zao.

Mfanyabiashara mmoja, Bw Duncan Nduati ambaye anaendesha biashara ya vifaa vya masuala ya kiteknolojia, alisema biashara nyingi zilizokuwa zikilipa Sh10,000 kwa mwaka kupata leseni na vibali muhimu, sasa zinalazimika kuchota Sh30,000.

“Sisi wafanyabiashara tunakaribia kufunga kwa sababu hatuwezi tena kufinywa zaidi ya hapo,” alilalamika Bw Nduati.

Bw Ben Mahui ambaye anauza bidhaa za kemikali na dawa za maabara, alisema siku hizi hakuna faida yoyote wanapata katika biashara hiyo kutokana na leseni ya juu inayotozwa na kaunti ya Kiambu.

Wafanyabiashara hao walisema baada ya kutoka kwa masaibu magumu ya janga la ugonjwa wa Covid-19 mwaka wa 2021 walipata afueni kidogo lakini kwa sasa mambo yamewalemea vilivyo.