Habari Mseto

Bidco Africa na MKU kwenye mkataba wa ushirikiano

February 4th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KAMPUNI ya Bidco Africa Limited na Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) zimeweka mkataba maalum ili kuona ya kwamba wahitimu wanajumuishwa katika ajira baada ya kukamilisha vipindi vya masomo yao.

Naibu Chansela MKU Prof Peter Wanderi alisema Jumatatu ushirikiano huo ni muhimu kwa sababu wahitimu wengi watapata mbinu ya kujitegemea na kuendesha biashara zao wenyewe.

“Tunataka kuona ya kwamba wanafunzi wanaokamilisha masomo yao wanakuwa tayari kukabiliana na ulimwengu ambao una ushindani mkubwa. Wachache watakaojiunga na Bidco Africa watakuwa na mwelekeo mzuri katika biashara,” alisema Prof Wanderi.

Aliyasema haya wakati wa kutia saini mkataba wa ushirikiano baina yao na kampuni ya Bidco Africa Ltd katika ukumbi wa seneti wa chuo hicho.

Alisema ushirikiano huo utaleta mabadiliko makubwa hasa kwa wahitimu wanaokamilisha masomo ya chuo kikuu.

Alisema kampuni ya Bidco Africa itakuwa mstari wa mbele kuwanoa wanafunzi hao wa MKU ambapo wataanza kuhamasishwa kwa kupewa mafunzo ya kibiashara pale wanapokuwa likizoni.

“Baadaye kampuni itawaajiri wale watakaojituma kwa njia inayostahili. Pia kuna wengine watalazimika kufungua biashara nje huku wakipewa bidhaa za kampuni kuuzia wateja,” alisema Prof Wanderi.

Mkurugenzi wa kampuni ya Bidco Africa Bw Chris Diaz alisema wanaunga mkono ajenda nne muhimu za serikali hasa ujenzi wa viwanda na maswala ya ajira.

“Tunaunga mkono serikali ujenzi wa vyuo vya kiufundi kote nchini ili kuwapa vijana nafasi nzuri ya kupata ajira hasa wanafunzi wanaokamilisha masomo yao,” alisema Bw Diaz.

Alisema wahitimu watakaojiunga na kampuni hiyo watapata nafasi kuelewa jinsi ya kuendesha biashara na pia kujitegemea wanapozindua biashara zao binafsi.

Uongozi wa Bidco na ule wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU). Picha/ Lawrence Ongaro

Ushirikiano huo utafanya juhudi kuona ya kwamba wanaendesha hafla za mafunzo kuhusu mauzo, na utafutaji wa soko kwa bidhaa za Bidco Africa Ltd.

Alisema kiwanda hicho kilibuniwa miaka 30 iliyopita ambapo kwa sasa kina matawi zaidi ya 15 katika bara la Afrika, huku kikiwa na mikataba ya kibiashara na nchi kadha za nje.

Hivi majuzi kiwanda hicho licha ya kutengeneza mafuta ya kupikia chakula na sabuni, kililenga pia kutengeneza vinywaji vya sharubati chapa Jooz, na Planet.

Chuo cha Mount Kenya kina idadi ya wanafunzi wapatao 40,000 kutoka vitengo tofauti maeneo tofauti. Baadhi ya vitengo vingine ni Mombasa, Nairobi Nakuru, na Meru.

Kampuni hiyo pia ina uhusiano wa karibu na wakulima mashinani huku pia wakishirikiana kwa kuwapa mafunzo jinsi ya kuendesha kilimo cha upanzi wa Corn Flowers.