Habari Mseto

Bidco Africa yawajali wagonjwa Thika

December 28th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kuwajali wagonjwa na wasiojiweza hasa wakati huu wa msururu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

Kampuni ya Bidco Africa Limited mnamo siku ya Krismasi ilizuru hospitali kuu ya Thika Level Five ambapo wanawake na watoto walipokea vinywaji.

Kwaya maalumu ya Bidco iliwatembelea wagonjwa hasa wanawake na kuwapa maji ya chupa na sharubati huku ikiwaimbia nyimbo za Krismasi.

Mwakilishi wa kampuni hiyo Bw Willys Ojwang’ alisema kampuni inaamini kusaidia wasiojiweza ambapo hiyo ni mojawapo ya mambo ambayo hufanywa kila mwaka.

“Licha ya kutembelea hospitali sisi pia hutembelea wafungwa gerezani, na wasiojiweza katika makazi yao. Hata wiki iliyopita kampuni ya Bidco ilizuru gereza la Kamiti na kuwafadhili wafungwa na zawadi tofauti,” alisema Bw Ojwang’.

Alitoa mwito kwa wahisani na wanaojiweza kifedha kuwa mstari wa mbele kuwapa watu wenye shida usaidizi wa dharura.

Kiongozi wa kwaya ya Bidco Bw Philip Mutunga alisema walikuwa mstari wa mbele kuwapa wagonjwa matumaini.

Kiongozi wa kwaya ya Bidco Bw Philip Mutunga alisema Desemba 24, 2019, kampuni hiyo huwa mstari wa mbele kuwapa wagonjwa matumaini. Picha/ Lawrence Ongaro

“Tayari leo (Desemba 24, 2019) tumewapa wanawake na watoto matumaini baada ya kuwatembelea hospitalini. Hata wiki iliyopita tulitembelea wafungwa katika gereza kuu la Kamiti ambapo tuliwaimbia na kuwapa zawadi,” alisema Bw Mutunga.

Alisema kampuni ya Bidco iko mstari wa mbele kuona ya kwamba wanawajali wagonjwa na wasiojiweza.

Mwanakwaya mwingine Bi Babra Ambani alisema kampuni hiyo imejitwika jukumu la kuwajali wote walio na shida.

“Mara kwa mara kampuni ya Bidco hutembelea watu wa tabaka mbalimbali kwa lengo la kuwapa tabasamu na kusherehekea sikukuu kama watu wengine,” alisema Bi Ambani.

Bi Janet Wafula ambaye alipelekwa hospitalini kujifungua mtoto anasema madaktari katika hospitali hiyo wanatekeleza jukumu lao bila ubaguzi.

“Tayari nimekamilisha siku mbili hapa na ninatarajia kuondoka wakati wowote,” alisema Bi Wafula.