Kimataifa

Biden ajiandaa kuingia Ikulu Trump akiendelea kulalamika

November 13th, 2020 2 min read

Na AFP

RAIS mteule wa Marekani Joe Biden jana aliendelea na maandalizi ya kuchukua rasmi uongozi wa taifa hilo licha ya Rais Donald Trump kukataa kukubali kushindwa kwenye uchaguzi wa November 3.

Biden alimtaja msaidizi wake wa miaka mingi Ronald Klain kama Mkuu wa Wafanyakazi katika Ikulu ya White House. Klain pia alihudumu kwenye wadhifa huo, Biden alipokuwa Makamu wa Rais kwa miaka 10 chini ya utawala wa Rais mstaafu Barrack Obama.

Klain anatarajiwa kushirikiana na kamati ya kitaifa ya kupokezana mamlaka huku Biden akitarajiwa kuapishwa rasmi mnamo Januari 20,2021.

Vilevile Klain atakuwa na kibarua kigumu kuhakikisha Biden anatekeleza sera thabiti za kusaidia kupambana na virusi vya corona na pia kuwaunganisha Wamarekani ambao wamegawanyika tangu matokeo yatolewe.

“Ana tajriba na ujuzi wa kufanya kazi na watu wote kutoka mirengo yote ya kisiasa. Nina imani tutafanya kazi pamoja naye kuhakikisha kuna umoja kati ya raia wa Marekani,” akasema Biden baada ya kufanya uteuzi huo.

Rais huyo mteule alitoa tangazo hilo baada ya kuweka shada la maua katika eneo la kumbukumbu la vita vya Korea, Philadelphia kama sehemu ya kusherehekea na kuwatambua wakuu walioshiriki vita hivyo.

Rais Trump naye alihudhuria sherehe kama hiyo kwenye makaburi ya Arlington, jijini Washington. Sherehe hiyo iliyofaa kuwa ya kitaifa na kuwajumuisha viongozi ilidhihirisha mgawanyiko mkubwa Marekani hasa baada ya Rais Trump kukataa kutambua ushindi wa Biden.

Rais Trump alionekana kwa mara ya kwanza hadharani wakati wa sherehe hiyo japo hakuhutubia umma jinsi ilivyotarajiwa.

Aidha Rais Trump amekuwa akitumia mitandao ya kijamii na taarifa zilizoandikwa kudai kuwa uchaguzi wa Marekani uligubikwa na udanganyifu huku chama chake kikiwasilisha kesi katika majimbo mbalimbali kupinga matokeo ya kura.

Rais huyo inaonekana ameanza kutelekeza majukumu yake huku visa vya virusi vya corona navyo vikiendelea kuongezeka.

Mara nyingi amekuwa akisalia Ikulu huku akidai anaelekea kushinda uchaguzi ambao matokeo yake yashatolewa.

Ingawa alishinda katika jimbo la Alaska na kujiongeza kura tatu za majimbo, idadi hiyo haikutosha kubatilisha ushindi wa Biden.

Baadhi ya maseneta wa Republican hata hivyo wametoa wito kwa kiongozi huyo kukubali matokeo wakisema pingamizi zake zinakiuka demokrasia na kulemaza mchakato wa kubadilisha mamlaka.

Katibu wa Republican katika jimbo la Montana Corey Stapleton alisema Rais Trump amewatendea raia wa Marekani mambo mengi na muda umefika aondoke baada ya kushindwa uchaguzini.

Hata hivyo, Katibu wa Masuala ya Nje Mike Pompeo na kiongozi wa Seneti Mitch McConnel wameunga mkono Rais Trump wakisisitiza kesi zilizowasilishwa kortini zitabadilisha ushindi wa Biden.

“Kutakuwa na upokezanaji wa mamlaka kutoka utawala wa Trump kwa muhula wa pili wa uongozi wake,” akasema Pompeo akisisitiza Rais Trump ndiye mshindi wa uchaguzi wa mapema mwezi huu.