Habari

Biden awataka Waamerika watulie wakisubiri matokeo ya uchaguzi

November 7th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MGOMBEA wa kiti cha urais Amerika kwa tiketi ya chama cha Democratic, Joe Biden ameelezea imani yake kuwa atashinda katika kinyang’anyiro cha wadhifa huo ambapo anatoana kijasho na Rais aliye madarakani, Donald Trump wa chama cha Republican.

Uchaguzi wa Amerika ulikamilika mnamo Jumanne, Novemba 3, 2020, huku mchakato wa kuhesabu na kujumuisha kura ukiendelea.

Matokeo ya ziada yanaonyesha Joe Biden anaongoza.

“Takwimu zinatuambia wazi tuko pazuri,” makamu huyo wa zamani wa Rais amesema kwenye hotuba yake kwa taifa kupitia vyombo vya habari Amerika.

Katika hotuba hiyo iliyopeperushwa moja kwa moja na vyombo vya habari Jumamosi, Biden alikuwa ameandamana na mgombea mwenza Kamala Harris.

Akiridhia kutwaa baadhi ya ngome zinazoaminika kuwa na ufuasi mkubwa wa Rais Trump, amesema Waamerika “walionichagua wanataka maendeleo.”

Majimbo ya Georgia, Arizona, Nevada na Pennsylvania yamekuwa chini ya chama cha Republican kwa muda mrefu, na ndiyo yanaaminika kumpa ushindi Rais Trump 2016 dhidi ya mpinzani wake Hillary Clinton aliyegombea kwa tiketi ya Democrats.

“Walioonyesha haki yao kushiriki uchaguzi na bila shaka wanataka maendeleo. Taifa lije pamoja, ila si kutengana. Tutaangazia suala la ugonjwa wa Covid-19, ukosefu wa kazi…” Biden akasema, akiahidi kuafikia ajenda alizoahidi Waamerika wakati wa kampeni.

Bila kutaja jina la Rais Trump, Biden amesema uchaguzi uliokamilika huku shughuli za kujumuisha kura zikiendelea, umekuwa kinyang’anyiro tu na kwamba “tumetofautiana kimawazo na kisiasa, sisi si maadui”.

“Nitahudumia walionichagua na wale ambao hawakunichagua,” akasisitiza.

Rais Trump ameashiria kupinga matokeo ya uchaguzi huo, akisema ataelekea katika mahakama ya juu zaidi.

Siku kadhaa zilizopita, alisema kumekuwa na udanganyifu katika uchaguzi huo, akisisitiza kuwa ana imani ameshinda, kuhifadhi kiti chake.

Tayari maandamano ya wafuasi wa Republican yameanza kushuhudiwa.