Habari Mseto

Bidhaa feki huipotezea serikali Sh200 bilioni – Ripoti

June 27th, 2018 1 min read

Na WANDERI KAMAU

SERIKALI hupoteza Sh200 bilioni kila mwaka kutokana na uingizaji wa bidhaa ghushi nchini.

Hii ni licha ya mikakati ambayo imekuwepo katika juhudi za kukabiliana na bidhaa hizo.

Hata hivyo, Mamlaka ya Kitaifa Kuhusu Bidhaa Ghushi Kenya (ACA) ilisema kwamba imefaulu kunasa bidhaa za Sh1.8 bilioni, tangu operesheni dhidi yake kuanza mwaka huu.

Kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa Kuhusu Bidhaa Ghushi jijini Nairobi jana, mamlaka ilisema kwamba imefaulu kuwakamata watu 1,200 kuhusiana na bidhaa hizo tangu mwaka 2011.

Akihutubu kwenye maadhimisho hayo, Afisa Mkuu Mtendaji wa mamlaka hiyo, Elema Halake, alisema kwamba serikali imeimarisha juhudi zake kukabili bidhaa hizo, kwani zinapunguza pato la jumla la kitaifa.

“Bidhaa hizo zimeisababishia serikali hasara kubwa, kwani wahusika huwa wanaingiza bidhaa hizo kwa njia haramu, ambapo huwa wanakwepa kulipa kodi,” akasema Bw Halake.

Kwa hayo, alieleza wameimarisha ushirikiano wao na asasi kama Polisi wa Kimataifa (Interpol), ubalozi wa nchi kadhaa kama Amerika na Uingereza kati ya nyingine ili kuwanasa wanaohusika.

Katibu wa Wizara ya Biashara na Viwanda, Chris Kiptoo alisema serikali imefanya mageuzi katika Sheria Dhidi ya Bidhaa Ghushi, ili kuziwezesha asasi husika kuimarisha ushirikiano wao kuwakabili wanaohusika.

Hayo yanajiri huku serikali ikiimarisha operesheni dhidi ya bidhaa hizo, chini ya uongozi wa jopo maalum lililobuniwa na Rais Uhuru Kenyatta, chini ya uongozi wa Naibu Mkuu wa Utumishi wa Umma Wanyama Musiambo.

Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i ameapa kuendeleza operesheni hiyo hadi pale bidhaa hizo zitaisha nchini.