Bidhaa zilizoundwa kwa maganda ya miwa, magazeti na vitabu kulinda mazingira

Bidhaa zilizoundwa kwa maganda ya miwa, magazeti na vitabu kulinda mazingira

NA SAMMY WAWERU

BIDHAA za plastiki zinakisiwa kuchukua miaka na mikaka kabla kuoza, zinapotupwa au kuzikwa udongoni.

Ni uhalisia unaochangia kuharibu udongo na zaidi ya yote mazingira.

Itakumbukwa kwamba mwaka 2017 serikali ya Rais Mstaafu, Uhuru Kenyatta ilipiga marufuku matumizi ya mifuko ya karatasi za plastiki.

Amri hiyo hata hivyo inaendelea kupuuzwa, baadhi ya wafanyibiashara wakitumia mifuko hiyo kufunga ama kupakia bidhaa.

Serikali ilitangaza kutoza faini watakaopatikana kukiuka sheria hiyo, Mamlaka ya Uhifadhi wa Mazingira Nchini (Nema) ikionekana kulegeza kamba.

Licha ya ulegevu huo, ulijua maganda ya miwa, magazeti, majarida na vitabu yanaweza kutatua suala la matumizi ya mifuko ya mizigo?

Shree Krishna Paper Mills and Industries Ltd, kampuni kutoka India ina jawabu hilo.

Mkurugenzi Mkuu, Sanjeev Singhai anadokeza kwamba shirika lake hutengeneza mifuko ya khaki, kwa kutumia magazeti, katoni na vitabu vilivyotupwa.

Sanjeev Singhai, Mkurugenzi Shree Krishna Paper Mills and Industries Ltd kutoka India akielezea kuhusu mifuko ya mizigo iliyoundwa kwa kutumia magazeti, katoni na vitabu vilivyotupwa. PICHA | SAMMY WAWERU

Vilevile, huunda mabahasha, bidhaa ambazo Singhai anasema teknolojia na uvumbuzi aliokumbatia ukitua nchini kero ya plastiki Kenya itakuwa historia.

Mifuko ya mizigo ni kati ya bidhaa zinazotumika kwa wingi nchini, hususan kwenye masoko na maduka.

“Baada ya magazeti, katoni na madaftari kutumika wengi hutupa, ila sisi tunazichakata (recycle,” asema afisa huyo.

Kampuni yake aidha ina soko tayari Amerika, Uingereza na katika mataifa ya Uarabuni (UAE), wakati wa Maonyesho ya Propaper Africa 2022, katika jengo la Kibiashara la Sarit Centre, Nairobi akifichua kwamba ameanza kupata oda za bidhaa Kenya.

Hafla hiyo ililenga kuonyesha bidhaa zilizotengenezwa kwa kutumia maganda ya miwa maarufu kama bagasse, magazeti na vitabu.

Bagasse, hutumika kuunda katoni za kupakia mizigo na sahani.

Sahani za kubebea mlo zilizotengenezwa kwa bagasse. PICHA | SAMMY WAWERU

Yashtech, kampuni kutoka Dubai inayomilikiwa na vijana wawili nao walionyesha sahani na vifaa vya kupakia na kubebea mlo vilivyoundwa kwa maganda ya miwa.

Maganda ya miwa – bagasse, yanayotumika kuunda makatoni ya kupakia mizigo na sahani. PICHA | SAMMY WAWERU

Meneja wa Mauzo, Sreerag Remesh akikadiria sahani hizo kugharimu kati ya Sh15 – 30 alisema zinatumika kupasha chakula moto kwa kutumia kikangazi (microwave).

“Tukumbatie matumizi ya sahani na bidhaa za kula zisizoharibu mazingira,” akahimiza.

Ni uvumbuzi na bunifu ambazo zikikumbatiwa nchini, mbali na kuokoa mazingira zitawapa wakulima hasa wa miwa mianya mbadala kujipa mapato.

Remesh alieleza imani yake kwamba Kenya inaweza kujinasua kutoka kwa minyororo ya matumizi ya bidhaa za plastiki.

  • Tags

You can share this post!

Wabunge wa Azimio wataka Chebukati, Guliye, Molu...

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Giroud afikia rekodi ya Thierry...

T L