Makala

BIDII YA NYUKI: Ujuzi wake katika kushona viatu huduwaza wengi

February 6th, 2020 3 min read

NA CHARLES ONGADI

NI kibanda kilichoko mkabala na duka kubwa la Tuskys, Mtwapa, Kaunti ya Kilifi ambako tunakutana na fundi Selina Mugulwa, 34, akiwahudumia wateja wake.

Kila mpita huishia kushangazwa na ufundi wa kushona viatu wa mama huyu wa watoto sita ambaye kaondokea kupendwa na wakazi wengi eneo la Mtwapa kutokana na ujasiri wake.

“Napenda kazi yangu kwa sababu ndiyo inayoniwekea chakula mezani kila siku na kazi ni kazi najivunia kuwa fundi wa pekee wa kushona viatu eneo hili,” asema Mugulwa.

Mugulwa ambaye ameajiriwa katika kibanda hiki na John Karisa, anafichua kwamba alijifunza kazi ya kushona viatu kutoka kwa mumewe ambaye ni fundi eneo la Kwale.

Kulingana na Mugulwa, mumewe aliamua kumfunza kazi ya kushona viatu baada ya kubaini kwamba alikuwa na wateja wengi waliohitaji huduma zake.

“Ijapo mwanzoni akina mama wenzangu walinishauri kutojihusisha na kazi hii ya kushona viatu wakidai ni ya wanaume, mwenyewe niliipenda kazi yenyewe kwa moyo wangu wote,” asema Mugulwa.

Hata hivyo, miaka miwili baada ya kujifunza kazi hii Mugulwa alikosana na mumewe na kulazimika kurudi kwao.

Haikuwa kazi rahisi kuwalea wanawe kwa kuwa hakuwa na njia yeyote ile ya kujipatia riziki na ndipo akaamua kupiga kiguu na njia hadi mjini Mtwapa kusaka kazi.

Ingawa mji wa Mtwapa unafahamika kuwa kituo cha starehe hasa kwa watalii wanaozuru nchini, Mugulwa aliapa kutojiingiza katika biashara ya ukahaba ambayo imekita mizizi eneo hili.

Alibahatika kuajiriwa kama yaya ila akaamua kuacha kazi hiyo baada ya kipindi kifupi baada ya kubaini kwamba haikuwa ikimletea tija maishani.

“Wanangu walihitaji kula na kwenda shule wakati kwa upande mwingine nikihitaji kulipa kodi ya nyumba niliyokodi,” asimulia Selina.

Licha ya kuwa na ujuzi wa kushona viatu, haikuwa rahisi kwake kufungua kibanda chake cha kushonea kutokana na bei ya juu ya kodi.

Lakini kama wasemavyo wavyele kwamba akili ni nywele na kila mmoja ana zake, aligundua kwamba idadi kubwa ya watu huwa na viatu vinavyohitaji kurekebishwa ila hawana muda wa kufika kwa fundi kufanyiwa marekebisho.

“Nilijipiga moyo konde na kuanza kujituma kwa kuwatembelea majumbani wakazi wa Mtwapa na maeneo jirani ya Shimo la Tewa na kuwashonea viatu vyao kwa bei nafuu,” asimulia.

Ni kazi aliyofanya kwa ustadi mkubwa na kipindi alipowaacha wengi kwa mshangao kama fundi wa kushona viatu wa kike ndivyo alivyozidi kujipatia wateja kibao.

Wengi walianza kumwita kuwashonea viatu majumbani mwao jambo lililomwezesha kuwawekea watoto wake chakula mezani kila siku.

Ni katika pilkapilka hizo za kuwahudumia wateja wake majumbani ndipo alikutana na John Karisa aliyemwomba kumuajiri katika kibanda chake kilichoko Mtwapa.

Kwa mujibu wa Mugulwa, Karisa alifurahishwa na kazi yake safi na kuamua kumwajiri katika kibanda chake.

Kulingana na Karisa, ustadi wa Mugulwa umewavutia wateja wengi wanaofurahika sana wanapohudumiwa na yeye kutokana na kwamba anamakinika kazini.

Hata hivyo, Mugulwa alidinda kuifichulia Akilimali kiasi anacholipwa kwa siku ila tu kusema kwamba mshahara anaopata umemweza kubadilisha maisha yake maradufu.

Dikson Mwandawiro ambaye ni kati ya wateja wa Mugulwa anasema kwamba yeye hupendelea sana kushonewa viatu na Mugulwa kwa sababu anamakinika zaidi.

“Ana ustadi wa kipekee wa kushona viatu kuliko baadhi ya mafundi wa kiume na hata wakati anapiga rangi viatu anamakinika na kung’arisha kwa kiwango kinachohitajika,” asema Mwandawiro.

Hata hivyo, katika kila kazi kuna changamoto zake ambapo Mugulwa anasema kwamba kuna baadhi ya wateja humchukulia kivyengine wanapomwona akifanya kazi hiyo inayomilikiwa na wanaume.

Asema kuna baadhi ya wateja huchukulia kwa kufanya kazi hiyo pengine kachanganyikiwa kimaisha na hutumia fursa hiyo kumrushia chambo kumtaka kimapenzi. Lakini Mugulwa asema mara nyingi huwashauri wateja wenye nia tofauti na kazi kuheshimu kazi yake.

Aidha, anasema kwa sasa anasaka mtaji kwa udi na ambari utakayomwezesha kuanzisha biashara yake ya kuwahudumia wateja wake.

“Hivi nikipata mtaji mzuri nitaweza kufungua kibanda changu cha kushona vyatu na kung’arisha vyatu kwa nia ya kubailisha maisha yangu maradufu kwa sababu nia na uwezo ninao,” asema.

Anawashauri akina mama kujiamini na kukubali kufanya kazi yoyote ile almradi ni halali na kujiepusha kuwategemea akina baba kwa kila jambo