Michezo

BILA KITITA HATOKI NG'O! Neymar atamani sana kuondoka PSG

August 23rd, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

PARIS, UFARANSA

PARIS Saint-Germain (PSG) imekataa ofa ya kwanza rasmi kutoka kwa Barcelona kwa mchezaji nyota wa Brazil, Neymar.

Barca imeshuhudia mpango wa kuchukua mshambuliaji huyo kwa mkopo ukikataliwa na miamba hao kutoka Ufaransa, gazeti la Marca nchini Uhispania limesema.

Mabingwa wa Uhispania, Barca, wanataka kumpa kandarasi tena mchezaji huyo uwanjani Nou Camp katika kipindi hiki cha uhamisho, lakini bei inayoombwa na PSG imekuwa tatizo kubwa.

Gazeti la Marca linadai kuwa Barcelona ilikubali kuchukua mshambuliaji huyu ambaye hajatulia uwanjani Parc des Princes wala kuchezea PSG msimu huu kwa mkopo halafu imenunue kabisa katika kipindi kirefu cha uhamisho mwaka 2020 kwa Sh17.1 bilioni.

Hata hivyo, mabingwa hawa wa Ligi Kuu ya Ufaransa wanaaminika wanaona thamani ya Neymar kuwa karibu na Sh28.6 bilioni, na pia wanataka hakikisho kutoka kwa mabingwa hao wa Uhispania kuwa watamsaini mwisho wa msimu huu.

Ripoti zinasema kuwa mazungumzo kati ya klabu hizi mbili bado hayajagonga ukuta, huku wote wakiendelea kuzungumza kuhusu uhamisho kabla ya soko kufungwa Septemba 2.

Hata hivyo, nafasi ya Barcelona kupata huduma za nyota huyo wao wa zamani imetatiziwa na shughuli yao wenyewe kununua wachezaji kadhaa wakiwemo Antoine Griezmann na Frenkie de Jong kwa fedha nyingi kumaanisha hawana budi kuangalia vitabu vyao vya fedha kwa makini kabla ya kukusanya fedha za kununua Neymar.

Nayo PSG inatafuta fedha za kuimarisha kikosi chake kwa hivyo haitakubali ofa ambazo italazimika kupunguza bei.

Ataka aruhusiwe kuhama

Neymar anatamani sana kuhama klabu hiyo kutoka jijini Paris baada ya kuwa mali yake kwa misimu miwili pekee.

Alitua PSG kutokea Nou Camp kwa Sh25.3 bilioni mwezi Agosti mwaka 2017.

Ameweka wazi kuwa anataka kurejea nchini Uhispania na ameachwa nje ya kikosi cha Thomas Tuchel kilichoshiriki mechi za ligi dhidi ya Nimes na Rennes.

PSG ilichapa Nimes 3-0 mnamo Agosti 11 kupitia mabao ya Edinson Cavani (penalti) na Kylian Mbappe na Angel Di Maria. Vijana wa Tuchel waliduwazwa 2-1 na Rennes mnamo Agosti 18 kupitia mabao ya M’Baye Niang na Romain Del Castillo yaliyopatikana dakika ya 44 na 48. Walifuta machozi kupitia bao la Cavani dakika ya 36.

PSG imeondoa matangazo yote yaliyo na picha ya Mbrazil huyu katika duka lake rasmi, huku mashabiki wa klabu hiyo wakiripotiwa kumtusi vibaya wakati wa mechi ya kuanza ligi dhidi ya Nimes.

Barcelona si klabu pekee iliyohusishwa na Neymar, bali pia kuna mahasimu wao wa tangu jadi Real Madrid. Ripoti pia zinadai kuwa miamba wa Italia, Juventus wanamezea mate Neymar na huenda wakatumia mshambuliaji kutoka Argentina, Paulo Dyabala kama chambo.