HabariSiasa

Bila Miguna, hakuna amani, wakazi Kisumu waimba

March 28th, 2018 2 min read

RUSHDIE OUDIA na EDDY ODHIAMBO

WAKAZI wa Kisumu Jumatano waliandamana katika eneo la Kondele, kulalamikia kuendelea kuzuiliwa kwa wakili Miguna Miguna katika uwanja wa Kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi.

Familia ya Miguna inayoishi Ahero eneobunge la Nyando pia ililalamikia jinsi mwana wao anavyonyanyaswa na serikali na kumtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati ili aachiliwe huru.

Waandamanaji walioanza kwa kusukuma mawe kufunga barabara inayounganisha miji ya Kisumu na Kakamega na kulazimisha wenye magari kutumia njia mbadala.

Waliimba “Bila Miguna, hakuna amani” na kubeba mabango wakitaka Miguna atendewe haki. Baadhi yao walichoma magurudumu ya magari na wengine kuvalia jezi zilizoandikwa kauli mbiu iliyobuniwa na wakili huyo ya “uasi.”

Familia ikiongozwa na kaka ya Miguna, Bw Ondiek Miguna, iliiomba serikali kumwachilia mwana wao kuingia nchini.

Dkt Miguna alifurushwa Kenya Februari lakini akarejea Jumatatu kufuatia agizo la korti la kumruhusu kuingia Kenya.

Hata hivyo, akiwa JKIA, alikataa kutoa paspoti yake ya Canada na kukataa kutia sahihi stakabadhi za kuomba uraia wa Kenya alizokabidhiwa na idara ya uhamiaji.

Ingawa idara hiyo inasema aliasi uraia wa Kenya miongo miwili iliyopita, Dkt Miguna anasema hakuwahi kuuasi na alizaliwa Kenya jambo linalompa haki ya kurudishiwa paspoti yake.

 

Huzuni

Bw Ondiek aliambia Taifa Leo kwamba familia inasononeshwa na jinsi Miguna anavyohangaishwa na polisi na serikali. Katika kijiji alichozaliwa cha Migina, wakazi walihuzunishwa na kuendelea kuzuiliwa kwake Nairobi.

“Hatujawahi kuwa na amani tangu Miguna alipokamatwa baada ya kumuapisha Raila Odinga hadi kisa cha hivi punde cha kuzuiliwa kwake. Baadhi yetu hatuli tukashiba tukisikiliza redio na kutazama runinga tukitarajia habari za kuachiliwa kwake,” alisema Bw Ondiek.

Wafuasi na familia ya Bw Miguna walisema wanahisi kusalitiwa na muungano wa NASA na mwafaka kati ya Rais na Bw Odinga.

“Tulifikiri mwafaka huo ungerahisisha mambo, ilhali wangali wanaendelea kuzuilia Miguna. Iwapo hawatamwachilia, tutakataa mwafaka huo na maridhiano,” alisema mwandamanaji mmoja.

Aliongeza: “Jaji Mkuu David Maraga anafaa kusimamisha shughuli zote za mahakama hadi maagizo ya korti yaheshimiwe”.