Habari Mseto

Bilionea Punjani arejea nchini kisiri

September 22nd, 2019 2 min read

Na MOHAMED AHMED

BILIONEA Ali Punjani ambaye amekuwa akitafutwa na polisi kwa madai ya kuhusika katika biashara ya dawa za kulevya, amerejea nchini kisiri na kujigamba kuwa hawezi kukamatwa.

Punjani alikuwa India polisi walipovamia maskani yake Agosti wakimtuhumu kwa kujihusisha na ulanguzi wa mihadarati.

Inadaiwa Bw Punjani aliingia kisiri nchini kupitia Tanzania wiki iliyopita na kujificha katika makao yake ya Nyali tangu wakati huo.

Haikubainika mara moja ni lini hasa Bw Punjani alirejea nchini.

Duru za kuaminika zilifichulia Taifa Jumapili kwamba maafisa wa polisi waliokuwa wakifuatilia kesi ya Bw Punjani walipewa maagizo thabiti kulegeza kamba kuhusiana na suala hilo kabla ya kurejea kwake nchini kutoka India ambapo anadaiwa alienda kusaka matibabu.

“Hatujui kuhusu kuwasili kwake nchini lakini maagizo yalikuwa wazi kwamba hapaswi kukamatwa,” zilisema duru miongoni mwa maafisa wa uchunguzi.

Mnamo Jumatatu, Bw Punjani alijigamba kuwa alikuwa mtu huru kinyume na ripoti zilizokuwa zimeenezwa kuwa polisi walikuwa wakimsaka ili kujibu mashtaka kuhusu ulanguzi wa dawa za kulevya.

Katika ujumbe kupitia mtandao wa WhatsApp kwa mwanahabari huyu, Bw Punjani alisema amekuwa Mombasa kwa wiki moja iliyopita.

“Niko Mombasa, nimekuwa mjini Mombasa kwa wiki moja na kama unavyoona, ninasoma gazeti la leo (siku ya mazungumzo) nyumbani kwangu,” akasema.

Aliongeza mengine.

“Niambie ni wapi na ni kituo kipi cha polisi ninachopaswa kwenda ili kuandikisha ripoti mara moja, ikiwa hilo litakukomesha kuzungumza kunihusu,” alisema huku akiwa amekerwa na maswali kuhusu iwapo alikuwa ameingia nchini kisiri kupitia mpaka wa Tanzania.

Kisha aliendelea kuthibitisha kuwepo kwake nchini kwa kuambatisha ujumbe huo na picha yake akiwa ameshika nakala ya gazeti la Daily Nation ya Septemba 16, akivalia kaptura nyeusi, koti jeusi na jezi nyeupe.

Ripoti kuwa aliingia nchini kisiri kupitia taifa jirani zilisambazwa mno mitandaoni na mwanablogu maarufu ambaye huchapisha sana matukio ya Pwani hasa yanayohusu usalama.

Alipoulizwa, Kamanda Mpya wa Polisi wa Kaunti ya Mombasa, Augustine Nthumbi, alijitenga na ilani iliyotolewa awali na watangulizi wake kwamba Punjani angekamatwa punde tu amgetua nchini.