Habari MsetoSiasa

Binamu ya Uhuru afagia kondoo wote sokoni

March 17th, 2019 1 min read

Na PIUS MAUNDU

WAANDALIZI wa mnada wa kondoo katika Kaunti ya Kajiado, walilazimika kuomba msamaha baada ya binadamu wa Rais Uhuru Kenyatta kununua mifugo wote waliokuwa wakiuzwa.

Bw Meshack Mbugua Muhoho, aliyefika sokoni hapo akiwa ameandamana na Spika wa Kaunti ya Kajiado Joseph Osoi, alinunua kondoo wote 12 kwa Sh390,000.

Mnada huo ulifanyika katika shamba la Paul Naigisie kijijini Erankau, Jumamosi.

Shirika la Dorper Sheep Breeders Society of Kenya, lililoandaa mnada huo kwa lengo la kuhamasisha wafugaji kukumbatia kondoo aina ya ‘dorper’, liliomba msamaha wakazi waliofika kununua mifugo hao.

Kondoo wa dorper walio na asili ya Afrika Kusini, hukua kwa haraka hata katika maeneo kame, na wanafaa zaidi kwa nyama yao ambayo ni nyororo.

Naibu Gavana wa Kajiado, Martin Moshisho alitumia mnada huo kuhimiza wakazi kufuga kondoo aina ya dorper ili waweze kujipatia mapato.

Aliwataka wakazi kufuga kondoo wachache wanaoleta mapato kuliko kuwa na mamia ya mifugo wasio na faida.

“Ni heri kuwa na kondoo wachache wa kisasa wanaoleta mapato makubwa kuliko kuwa na maelfu ya mifugo wasioleta kipato,” akasema Bw Moshisho.

Waziri wa kilimo wa Kaunti ya Kajiado, Jackline Koin alisema serikali ya kaunti inashirikiana na Idara ya Ustawi wa Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP) kulinda kondoo wekundu wa Kimaasai ambao wanapatikana tu miongoni mwa Wamaasai.