Dimba

Bingwa Faith Kipyegon apiga hatua kubwa akifukuzia kunyaka taji la 5,000m Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE August 2nd, 2024 1 min read

BINGWA wa dunia mbio za mita 5,000, Faith Kipyegon amepiga hatua muhimu katika juhudi za kutwaa taji lake la kwanza katika umbali huo kwenye Olimpiki baada ya kutinga fainali kwa kishindo jijini Paris nchini Ufaransa, Ijumaa.

Wakenya wenzake Margaret Chelimo na bingwa wa Jumuiya ya Madola 5,000m Beatrice Chebet pia wamefuzu kushiriki fainali Agosti 5.

Kipyegon, 30, ambaye anajivunia mataji matatu ya dunia ya watu wazima katika 1,500m na pia ni bingwa mara mbili wa Olimpiki katika 1,500m, alinyakua tiketi ya 5,000m kwa kushinda mchujo wa kwanza kwa dakika 14:57.56 baada ya kufyatuka katika kona ya mwisho.

Amefuzu pamoja na Mholanzi Sifan Hassan (14:57.65), Mwitaliano Nadia Battocletti (14:57.65), Chelimo (14:57.70), Waethiopia Gudaf Tsegay (14:57.84) na Ejgayehu Taye (14:57.97) na Waamerika Elise Cranny (14:58.55) na Karissa Schweizer (14:59.64). Sifan ndiye bingwa mtetezi.

Bingwa wa Michezo ya Jumuiya ya Madola Beatrice Chebet, ambaye alizoa nishani ya shaba kwenye Riadha za Dunia mjini Budapest nchini Hungary mwaka jana, alishiriki mchujo wa pili na kufuzu baada ya kukata utepe kwa 15:00.73 baada ya kuchukua uongozi ndani ya mita 100 za mwisho.

Muethiopia Medina Eisa (15:00.82), Rose Davies (15:00.86), Karoline Grovdal kutoka Norway (15:01.14), Francine Niyomukunzi kutoka Burundi (15:01.42), Mwamerika Whittni Morgan (15:02.14), Nathalie Blomqvist kutoka Finland (15:02.75) na Joselyn Brea kutoka Venezuela (15:02.89) walifuzu kwa kukamilisha nafasi nane za kwanza, mtawalia.

Vivian Cheruiyot, 40, anasalia Mkenya wa pekee kuwahi kushinda dhahabu ya 5,000m katika Olimpiki alipoongoza Mkenya mwenzake Hellen Obiri kufagia nafasi mbili za kwanza mwaka 2016 mjini Rio de Janeiro, Brazil.

Kipyegon pia atashiriki mbio za 1,500m hapo Agosti 6 ambazo anafukuzia taji la tatu mfululizo baada ya kutawala mwaka 2016 na 2020 nao Chelimo na Chebet watatimka katika 10,000m hapo Agosti 9.

Ratiba (Agosti 3):

Mbio za 100m wanaume (11.35am),

Mbio za nusu-fainali 100m wanawake (8.50pm),

Mbio za fainali ya 4x400m mseto (9.55pm)

Mbio za fainali ya 100m wanawake (10.20pm)

Mchujo wa uogeleaji – Maria Brunlehner (12.16pm)

Voliboli – Malkia Strikers (2.00pm)