Michezo

Bingwa Kipchoge kuongoza uwindaji dhahabu Olimpiki

January 31st, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MSHIKILIZI wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42, Eliud Kipchoge anatarajiwa kuongoza orodha ya wakimbiaji watakaopeperusha bendera ya Kenya kwenye Olimpiki 2020.

Shirikisho la Riadha nchini (AK) linapanga kutangaza timu imara itakayowakilisha taifa mjini Tokyo nchini Japan kwenye marathon ya wanawake itakayofanyika Agosti 2 na marathon ya wanaume itakayoandaliwa Agosti 9.

Kipchoge alishindia Kenya dhahabu yake ya pili ya marathon ya wanaume katika historia ya Olimpiki mwaka 2016 mjini Rio de Janeiro. Mwendazake Samuel Wanjiru alinyakua dhahabu mwaka 2008 mjini Beijing, Uchina. Kipchoge ameshinda marathon 11 kati ya 12 zinazotambuliwa na Shirikisho la Riadha Duniani ikiwemo ile ya Berlin 2018 alipotimka umbali huo kwa rekodi ya dunia ya saa 2:01:39.

Mwaka jana, Kipchoge alinyakua ubingwa wa London Marathon kwa saa 2:02:37 mwezi Aprili kabla ya kufunga mwaka kwa kuwa mtu wa kwanza kukimbia kilomita 42 chini ya saa mbili alipokamilisha mbio maalum za INEOS 1:59 Challenge kwa saa 1:59:40 mjini Vienna nchini Austria mwezi Oktoba.

Alitawazwa mwanariadha bora duniani mwaka 2018 na 2019.

Mwaka 2019 Kipchoge, 35, pia aliibuka mshindi wa tuzo ya Marathon Kuu Duniani (WMM) kwa mwaka wa nne mfululizo. Yeye ndiye mwanamichezo bora nchini Kenya 2019 baada ya kupokea tuzo hiyo kwenye tuzo za kifahari za SOYA mjini Mombasa wiki moja iliyopita.

Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya wanawake ya mbio za kilomita 42, Brigid Kosgei pia anatarajiwa kuwa katika orodha ya watimkaji watakaowakilisha Kenya katika marathon mjini Tokyo.

Kosgei, 25, alishinda Chicago Marathon nchini Marekani kwa saa 2:14:04 mwezi Oktoba mwaka jana. Kenya ilishinda taji la wanawake kwenye Olimpiki za Rio kupitia kwa Jemima Sumgong, ambaye hawezi kutetea ubingwa wake baada ya kupigwa marufuku 2017 kwa kupatikana alitumia dawa za kusisimua misuli.

Mbali na kutangaza kikosi cha Kenya kitakachotimka katika marathon mjini Tokyo, AK pia ilisema jana kuwa itasaini mkataba na wadhamini Lotto. Kampuni ya Lotto itafadhili mbio za nyika za kitaifa zitakazofanyika Februari 8 uwanjani Uhuru Gardens jijini Nairobi.

Wakati huo huo, bingwa wa Tokyo Marathon Valery Aiyabei na Milano Marathon Titus Ekiru wako katika orodha ya Wakenya watakaoshiriki mbio za Tokyo Marathon hapo Machi 1. Mshindi wa mwaka 2018 Dickson Chumba, pia kutoka Kenya, yuko katika orodha hiyo.